Post Details

ONGOZENI KWA MFANO: JAJI KIONGOZI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama Kanda ya Iringa kuongoza kwa mfano ikiwa ni pamoja na kuondosha mashauri kwa wakati.

Mhe. Jaji Kiongozi alitoa maelekezo hayo Aprili 06, 2019 alipokuwa akizungumza na Mahakimu Wafawidhi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, Mahakama ya Wilaya Iringa, Mahakama ya Wilaya Mufindi, Mahakama ya Wilaya Makete, Mahakama ya Wilaya Kilolo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama ya Wilaya Njombe.

Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliwaelekeza Mahakimu hao Wafawidhi kusimamia na kuhakikisha kuwa mashauri yanaamuliwa kwa wakati sanjari na kuhakikisha kuwa nakala za hukumu zinachapwa na kukabidhiwa kwa wadaawa na wadau bila kuchelewa.

“Nyote mnaelewa kuwa Mahakama imejiwekea malengo katika usikilizaji wa mashauri, hivyo ni wajibu wenu kusimamia malengo ambayo yameelekezwa kupitia nyaraka mbalimbali za Mahakama, kwahiyo ni muhimu kujituma ili kufikia malengo husika,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.

Mhe. Jaji Kiongozi aliuagiza pia Uongozi wa Mahakama Kanda ya Iringa kutoishia tu kupokea taarifa za mashauri bali kupata suluhisho kwa Mahakama ambazo hazifanyi vizuri katika uondoshaji wa mashauri.

“Ninyi ni Viongozi, mkiona vitu havitekelezeki au kama kitu kinashindikana jiulize tatizo ni nini, na kama tatizo ni sheria jengeni hoja sheria husika zirekebishwe,” alisisitiza Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.

Aliongeza kuwa kama Hakimu ameshindwa kufikia malengo yaliyowekwa anapaswa kutoa taarifa na kueleza sababu zilizochangia kutofikia malengo husika ili utatuzi upatikane kuanzia ngazi ya kituo husika mpaka ngazi ya Kanda na ikishindikana ifikishwe ngazi ya Makao Makuu kwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Jaji Panterine Kente alimuhakikishia Mhe. Jaji Kiongozi kuwa wamepokea maelekezo yote aliyoyatoa na kuahidi kushughulikia vikwazo vyote ili kusonga mbele.

Mhe. Jaji Kiongozi yupo ziarani kikazi katika Mahakama Kanda ya Iringa na anatarajia kufanya ziara pia katika Mahakama Kanda ya Mbeya lengo likiwa ni kujua  hali ya maendeleo ya utekelezaji wa maboresho ya huduma mbalimbali za Mahakama na vilevile kuwakumbusha Watumishi wa Mhimili huu kuendelea kutekeleza jukumu la msingi la utoaji haki nchini kwa ubora wa hali ya juu kwa manufaa ya wananchi ambao ndio walengwa wakuu.

Comments (0)

Leave a Comment