Post Details

MAHAKAMA YAFANIKIWA KUMALIZA MASHAURI KWA ASILIMIA 98.7

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama, Mbeya

Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kusikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 87,116 sawa na asilimia 98.7 ya mashauri 88,232 yaliyosajiliwa katika ngazi zote za Mahakama katika kipindi cha Januari na Mei mwaka huu.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya wakati wa Mkutano kati ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na watumishi hao, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza watumishi wote wa Mahakama kwa utendaji kazi mzuri uliotukuka kufuatia kusikilizwa kwa mashauri hayo.

Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo alisema Mahakama Kuu zote nchini zimefanikiwa kumaliza mashauri kwa asilimia 98. Alisema, kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye Taarifa ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, mashauri 5,848 yalisikilizwa na kumalizika kwenye kanda zote za Mahakama Kuu nchini kati ya Januari na Mei, 2021. Mashauri yaliyosajiliwa katika kipindi hicho yalikuwa ni 5,875.

Kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Jaji Mkuu alisema jumla ya mashauri 3,650 yalifunguliwa kati ya mwezi Januari na Mei, 2021 ambapo mashauri 4,320 yalisikilizwa na kumalizika sawa na asilimia 118. Alisema Mahakama hizo zimepunguza mlundikano wa mashauri kwa asilimia 18.

Kuhusu Mahakama za wilaya, Jaji Mkuu alisema zimefanikiwa kwa asilimia 96 kusikiliza na kumaliza mashauri yaliyosajiliwa kati ya mwezi Januari na Mei mwaka huu.  Jumla ya mashauri 15,598 kati ya mashauri 16,067 yaliyosajiliwa katika kipindi hicho yalisikilizwa.

Aidha, Mahakama zote za Mwanzo zimefanikiwa kwa asilimia 98 kusikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 61,005 kati ya mashauri 61,931 yaliyosajiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wa Mahakama za Watoto, Jaji Mkuu alisema zimefanikiwa kwa asilimia 100 kusikiliza na kumaliza mashauri yote yaliyosajiliwa kati ya kipindi cha Januari na Mei mwaka huu. Jumla ya mashauri 332 yaliyohusu Watoto yalisikilizwa na kumalizika. Mashauri yaliyosajiliwa katika kipindi hicho yalikuwa ni 329.

Jaji Mkuu alisema licha ya mafanikio makubwa ya Mahakama katika usikilizaji wa mashauri, bado Mhimili huo unakabiliwa na changamoto ya kutotumika ipasavyo kwa njia ya usuluhishi katika kuamua migogoro mbalimbali kwenye jamii. Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza matumizi ya njia hii na endapo itatumika itasaidia kupunguza idadi ya mashauri yanayofunguliwa mahakamani.

Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni kutokufungwa kwa mashauri ya mirathi yanayofunguliwa. Alisema kati ya mashauri 31,461 yaliyofunguliwa kwa nchi nzima, mashauri 28,130 hayajafungwa mpaka sasa hali inayoweza kusababisha wasimamizi wa mirathi kuendelea kufaidika na mali za marehemu.

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara katika mikoa ya Mbeya na Songwe kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu kwa wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau wa Mahakama.

 

Comments (0)

Leave a Comment