Post Details

SIMAMIENI VIAPO VYENU: JAJI MSTAAFU SHANGALI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Mary Simbo Shangali ametoa wito kwa Majaji na Mahakimu waliopo katika Utumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia viapo vyao.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Aprili 05, 2019 mara baada ya hafla ya kuagwa rasmi kitaaluma, iliyofanyika Mahakama Kuu Iringa, Mhe. Jaji Mstaafu Shangali alisema kuwa ni vyema kutekeleza majukumu kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

“Katika usikilizaji wa kesi ni vyema kumshirikisha Mungu na kusimamia viapo, hivyo tusicheze na mambo ambayo tumeapa mbele za Mungu tunapotekeleza majukumu yetu,” alieleza Mhe. Jaji Mstaafu Shangali.

Aidha; Mhe. Jaji Shangali aliwatia moyo Majaji na Mahakimu Wanawake  nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi na sheria zilizopo bila kuteteleka.

“Kuwa Jaji mwanamke kwa nchi zetu za Afrika si kazi rahisi kutokana na baadhi ya mila desturi zilizopo, kwa hiyo ni vyema wanawake kutekeleza na kusimamia haki bila kuteteleka,” alisema Jaji Shangali.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Shangali alitoa wito kwa jamii kuelewa kuwa pindi unapokuwa na kesi Mahakamani kuna kushinda au kushindwa, hivyo ni vyema kukubaliana na matokeo.

“Haki sio kushinda bali ni kupata kile unachostahili, kudai kwamba umenyimwa haki sio lugha sahihi, lazima upande mmoja utashinda na mwingine utashindwa,” alisema Jaji Shangali.

Kwa upande wake Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi aliyeongoza hafla hiyo alimuelezea Mhe. Jaji Mstaafu Shangali kuwa alikuwa mchapa kazi na mara zote alisimamia haki.

“Mhe. Jaji Mstaafu Shangali ni mfano mzuri wa wachapakazi, amefanya kazi vizuri na hadi kufikia mwisho hakuna jalada lolote la kesi aliloacha bila kukamilisha na huu ni mfano mzuri,” alisisitiza Mhe. Jaji Kiongozi.

Mhe. Jaji Mstaafu Shangali, alianza kazi Mahakama ya Tanzania mwaka 1983, ambapo katika utumishi wake alishika nafasi mbalimbali na hadi anastaafu Mhe. Jaji Shangali alikuwa Jaji namba. 1 wa Mahakama Kuu ya Tanzania na vilevile Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, na kufanya jumla ya miaka 35 ya Utumishi wake ndani ya Mahakama.

Comments (0)

Leave a Comment