Post Details

KUMBUKUMBU ZINAVYOIMARISHA HAKI KATIKA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

KATIKA maboresho mbalimbali ya huduma zake, Mahakama ya Tanzania inaendelea kufanya jitihada kadhaa kuhakikisha huduma zake zinakuwa bora zaidi.

Katika makala haya, tutaangazia maboresho katika utunzaji bora wa kumbukumbu ndani ya mahakama.

Katika mhimili wa mahakama, suala la utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu kwani kwa asilimia kubwa, mahakama inafanya kazi kwa kutumia kumbukumbu zinazohifadhiwa kimaandishi.

Kwa umuhimu huu, masjala ndiyo kitovu kikuu katika uendeshaji wa mahakama kwa kuwa baadhi ya kumbukumbu huhifadhiwa huko.

Katika mahojiano maalumu na Mkurugenzi wa Kumbukumbu, Mahakama ya Tanzania, Malimo Manyambula anasema neno kumbukumbu linatokana na neno la Kilatini lijulikanalo kama ‘recordum’ ikiwa na maana ya ushuhuda wa shahidi (testimony of witness).

Manyambula anazidi kulielezea neno kumbukumbu akisema ni taarifa ya kimaandishi inayopokelewa au kuzaliwa na taasisi husika ili kusaidia taasisi hiyo kutoa uamuzi sahihi na kwa wakati mfupi iwezekanavyo.

Katika kuendeleza  utunzaji bora wa kumbukumbu, Mahakama ya Tanzania kwa kuzingatia umuhimu wa suala hili, imeanzisha Kurugenzi maalumu ya kumbukumbu ili kuwa na usimamizi na utunzaji bora wa kumbukumbu tangu inapozaliwa/kufunguliwa hadi inapofungwa.

Kadhalika, kutoa ushauri, mafunzo na kuweka mifumo kwa kutumia viwango vya ndani na vya kimataifa.

Hivi karibuni Mahakama ya Tanzania kupitia Kurugenzi hii ilifanya uchambuzi maalumu, kuorodhesha na kuweka katika maboksi mafaili yaliyofungwa (closed case files) katika mahakama 12 zilizopo mkoani Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Manyambula, jijini Dar es Salaam kazi hiyo ilifanyika katika Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

Nyingine ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Mahakama ya Hakimu Mkazi Jiji/ Kivukoni na katika mahakama za wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni.

Mkurugenzi huyo anasema Mahakama imekuwa ikizalisha kumbukumbu nyingi kutokana na utendaji kazi wake, hivyo mashauri yanapokuwa yameisha/ yamefungwa kunakuwa na mlundikano wa mafaili yaliyomaliza muda wake.

“Mlundikano wa majalada una changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutumia muda mrefu na nguvu kubwa katika kutafuta majalada, kujaza nafasi za ofisi ambavyo vyote kwa jumla husababisha kuchelewa kwa matokeo chanya katika utendaji kazi,” anasema Manyambula.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kazi hiyo iliyoanza Januari 14 na kukamilika Februari 09, 2019, jumla ya majalada 225,150 yalichambuliwa na kufungwa katika maboksi 5,574.

Taarifa inaonesha idadi ya majalada yaliyochambuliwa na kufungwa huku kwa upande wa Mahakama ya Rufani jumla ya majalada 16,516 yalichambuliwa, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam majalada 31,628 yalichambuliwa, Mahakama Kuu Masjala Kuu majalada 270 yalichambuliwa.

Kwa upande wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara jumla ya majalada 2,798 yalichambuliwa, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi majalada 6,135, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi majalada 13, 213 huku Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiwa na jumla ya majalada 38,606 yaliyochambuliwa.

Aidha; kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni ambapo zoezi hili pia lilifanyika, jumla ya majalada 35,520 yalichambuliwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive jumla ya majalada 20,448 yalichambuliwa, Mahakama ya Wilaya Kinondoni  majalada 4,320, Mahakama ya Wilaya Ilala, majalada 28,838 na Mahakama ya Wilaya Temeke majalada 26,858.

Manyambula anaongeza kuwa, majalada yaliyochambuliwa na kufungwa katika maboksi yalipelekwa katika Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu za Serikali (National Archives) kilichopo jijini Dodoma.

Akizungumzia faida za kazi hiyo, Manyambula anasema inasaidia kutoa nafasi kwa majalada yanayotumika kuhifadhiwa vizuri, kupata majalada yanayohitajika kwa haraka na kwa wakati, kupunguza upoteaji wa majalada usio wa lazima na kuokoa nafasi katika ofisi iliyokuwa inachukuliwa na mlundikano wa mafaili.

Faida nyingine ni pamoja na kutambua kumbukumbu zitakazokuwa sehemu ya urithi andishi ‘written heritage’ na kujenga imani kwa wateja na wadau wengine wa mahakama.

Aidha; baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya kazi hiyo, Kurugenzi ya Kumbukumbu imejipanga kufanya zoezi hili katika Kanda 4 za Mahakama Kuu ambazo ni Dodoma, Mwanza, Arusha na Tanga.

“Matarajio tuliyo nayo kwa mwaka ujao wa fedha ni kuendesha zoezi hili katika kanda zote za Mahakama na mikoa.”

“Idara itaendelea kutoa ushauri kwa Mahakama ili kuendelea kutunza vizuri kumbukumbu na kuweka mifumo ya uendeshaji na udhibiti,” anasema Manyambula.

Mbali na hayo, Idara pia imejipanga kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa masjala kwa kuwapa mafunzo ya muda mfupi na mrefu ili wawe na weledi wa kutosha kusimamia vyema utunzaji wa kumbukumbu.

“Kuhusu mafunzo, watumishi 20 wamehudhuria Kongamano la Watunza Kumbukumbu lililofanyika mwezi Oktoba, 2018 mkoani Tanga…. Aidha, watumishi 13 wameshikizwa (attachment) kwenye aasisi saba ili kupata uzoefu wa utunzaji wa kumbukumbu na menejimenti ya masijala,” anasema mkurugenzi huyo.

Vilevile kuendesha vikao/semina kwa watendaji na watumiaji wa kumbukumbu ili waelewe matakwa ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika usimamizi wa kumbukumbu.

Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/ 2016 hadi 2019/2020), imelenga kuboresha huduma zake katika nyanja mbalimbali ili kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati kama isemavyo dira yake.

Mwandishi wa Makala hii ni Bi. Mary Gwera, Afisa Habari-Mahakama ya Tanzania.

 

Comments (0)

Leave a Comment