Post Details

JAJI MKUU AWATAKA MAHAKIMU WAKAZI WAFAWIDHI KUSIMAMIA MATUMIZI YA TEHAMA

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu Wakazi Wafawidhi kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwenye shughuli mbalimbali za Mahakama ikiwemo usikilizaji wa mashauri.

Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi hati za uteuzi Mahakimu wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Musoma na Simiyu jana jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu aliwataka Mahakimu hao kufanya shughuli zao nyingi kwa kutumia Tehama ili kurahisisha na kuboresha utendaji wao wa kazi.

“Matumizi ya Tehama ni moja ya eneo linalotakiwa kutubadilisha sisi katika utendaji wetu wa kazi, hivyo kuweni mstari wa mbele ili kufanikisha Mahakama Mtandao”, alisema Jaji Mkuu.

Aidha Jaji Mkuu amewashauri Mahakimu walioapishwa kutumia Teknolojia hiyo katika kutatua changamoto watakazokutana nazo kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ikiwemo ile ya upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali mahakamani.

Jaji Mkuu pia amewashauri Mahakimu hao kujenga tabia ya kujisomea hasa nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama ili wawe na uelewa mpana utakaowawezesha kuwaelimisha watumishi watakaowaongoza masuala mbalimbali ya kimahakama.

“Mahakama ina nyaraka nyingi, someni, eleweni, chambueni na kuzisambaza kwa watumishi walio chini yenu ili dhana ya maboresho ya huduma za Mahakama ieleweke na kufahamika kwa wanachi wengi zaidi”, alisisitiza Jaji Mkuu.

Alisema pamoja na majukumu mengine waliyonayo, Mahakimu Wafawidhi wote hawana budi kuwa mstari wa mbele katika kusimamia kwa umakini utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama pamoja na program ya maboresho ya huduma za Mahakama katika maeneo yao ya kazi.

Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru amewataka Mahakimu hao kutenda haki wanaposikiliza mashauri ya aina yote ili kujenga imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama na kushirikiana vizuri na viongozi wa Serikali katika maeneo yao.

Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka Mahakimu hao kusimamia suala la maadili kwa watumishi wanaowaongoza na kuhakikisha wanabuni mikakati mbalimbali itakayowezesha kumalizika kwa mlundikano wa mashauri mahakamani.

Mahakimu Wakazi waliokabidhiwa hati za uteuzi na Mhe. Jaji Mkuu ni Mhe. Frank Mushi aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Kinondoni ambaye sasa anakuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma. Mwingine ni Mhe. Judith Kamala aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Same na sasa ameteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment