Post Details

JAJI MFAWIDHI KIGOMA AZINDUA KAMATI YA NIDHAMU YA KANDA

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta amezindua rasmi kamati ya Nidhamu kwa watumishi wasio Maafisa wa Mahakama ili kushughulikia masuala ya kimaadili kwa watumishi wa Kanda hiyo.

Akizindua rasmi Kamati hiyo Juni mosi, 2021, Mhe. Jaji Mugeta alisema kuwa awali masuala yote ya nidhamu  yalikuwa yanashughulikiwa makao makuu ambapo jukumu la kanda lilikuwa ni kukusanya taarifa na kuzituma makao makuu ambao wao walikuwa na jukumu la kutoa maelekezo kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa Umma.

Aliongeza kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa mamlaka iliyokabidhiwa chini ya kifungu cha 33(1) cha Sheria ya uendeshaji wa Mahakama Na 4 ya mwaka 2011 imekasimu sehemu ya jukumu la usimamizi wa nidhamu kwa watumishi wasio maofisa wa Mahakama kwa kamati zilizoundwa katika ngazi ya makao makuu, Mahakama Kuu Masjala Kuu, Kanda na Divisheni zilizoanzishwa chini ya kanuni ya 19(1) (a) na (b) ya kanuni za uendeshaji wa Mahakama.

“Nidhamu ya watumishi ni eneo muhimu sana kwenye kuwezesha utumishi wa Umma kuwa na utumishi wenye tija. Nidhamu na maadili vikivurugwa basi huduma kwa wananchi zitakuwa duni.  Hivyo tunaitegemea kamati yenu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia sheria ili kuepusha manung’uniko ya kuonea au kupendelea watu ili hatimaye haki itakayokuwa ikipatikana katika kamati hii iwe ni haki dhahiri” alisema Jaji Mugeta

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka aliainisha majukumu ya kamati hiyo kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Mahakama kuwa ni pamoja na kufanya uchunguzi wa awali ili kubaini ukweli (facts) wa kosa ambalo mtumishi anatuhumiwa kulitenda, kumfungulia mashtaka au kutoa adhabu ikiwa mazingira yanaruhusu kufanya hivyo na kuunda kamati ya uchunguzi (Inquiry committee)” .

Baada ya kamati kuzinduliwa,  imeanza kazi rasmi kwa kushughulikia shauri moja la kinidhamu lililofikishwa mbele ya kamati. Aidha kamati imejipanga kuhakikisha inatoa elimu kwa watumishi kabla hawajafikishwa mbele ya kamati.

Maboresho yanayoendelea ndani ya Mahakama hususani ushushaji wa baadhi ya majukumu katika ngazi mbalimbali yanalenga kuboresha huduma na kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu.

 

Comments (0)

Leave a Comment