Post Details

JIFUNZENI ZAIDI MATUMIZI YA TEHAMA KUENDANA NA WAKATI; JAJI MKUU

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma amewapongeza Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kutoa huduma ya haki kwa wananchi huku akiwataka kuendelea kujifunza juu ya maendeleo ya TEHAMA kwa kuwa dunia ndipo ilipo kwa sasa.

Akifungua rasmi kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama mapema Mei 20, 2021 katika Ukumbi wa ‘Treasury Square’ jijini Dodoma, Mhe. Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo alisema ili kuendana na mabadiliko ya mapinduzi ya nne ya viwanda (4th industrial revolution) ambayo yamejikita zaidi katika matumizi ya TEHAMA ni muhimu Watumishi kuwa tayari kuendelea kujifunza kwa kuwa Mahakama ina dhamira ya kuendana na mabadiliko hayo.

“Naomba niwapongeze Watumishi wa Mahakama kwa kuendelea kufanya kazi nzuri licha ya changamoto mbalimbali, vilevile napenda kuchukua fursa hii kuwataka kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuwa dunia kwa sasa ipo katika Mapinduzi wa nne (4) ya Viwanda (4th Industrial Revolution) hivyo tujitahidi kufanya kazi ndani ya mapinduzi haya ili kutoa haki kwa wakati,” alisema Jaji Mkuu.

Aliongeza kuwa, hivi sasa Mahakama ipo tayari na imeanza kutumia TEHAMA katika shughuli zake mbalimbali ikiwemo kuwa na Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri kwa njia ya Kielekroniki, Mfumo wa Usimamizi na Uratibu wa Mawakili (TAMS) na kadhalika, hivyo ni muhimu Wafanyakazi kuwa tayari kuunga dhamira ya kuwa na Mahakama mtandao kwa manufaa ya wananchi.

“Barabara ya kuelekea katika Mahakama mtandao tayari imeshawekwa, na baadhi ya Mahakama ikiwemo Mahakama ya Wilaya Kigamboni tayari zimeanza kufanya kazi kielektroniki, hivyo ni muhimu Wafanyakazi kuendelea kupatiwa mafunzo ya TEHAMA ili kwenda na wakati ikiwa ni pamoja na kulinda ajira zenu kufuatia ukweli kuwa kutokana na utandawazi vitu vingi vitakuwa vikifanyika kielektroniki,” alisisitiza Mhe. Jaji Prof. Juma.

Akizungumzia hali ya uendeshaji wa mashauri, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa  Mahakama imefanya kazi kubwa ya kusikiliza na kuamua mashauri ambayo ni pamoja na yale ya zamani ambayo yamekuwa ni chanzo cha malalamiko na kupoteza imani kwa Wananchi wenzetu.

“Hadi kufika Disemba 2019, mashauri 66,873 yalibaki katika ngazi zote za Mahakama. Katika kipindi cha mwaka 2020 jumla ya mashauri 238,766 yalifunguliwa na Mashauri 243,464 yalisikilizwa sawa na asilimia 102 ya mashauri yote yaliyofunguliwa katika kipindi hicho,” alifafanua Mhe. Jaji Prof. Juma.

 

Alikiri kuwa hilo ni ongezeko la asilimia 2 katika usikilizwaji wa mashauri ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo yalifunguliwa mashauri 270,359 na kusikilizwa mashauri 269,513 sawa na salimia 100 ya mashauri yaliyofunguliwa Mahakamani katika kipindi hicho.

 

Kwa upande mwingine, akizungumzia juu ya maslahi ya Wafanyakazi wa Mahakama, Mhe. Jaji Mkuu ameahidi kuwa Mahakama itaendelea kuboresha maslahi ya Watumishi wake kadri inavyowezekana.

Kuhusu malimbikizo ya mishahara, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa hadi sasa Mahakama imepokea jumla ya malalamiko 1965 kutoka kwa watumishi ambapo madai 1756 yamewasilishwa kwa Katibu Mkuu Utumishi, na kati ya hayo madai 399 yamelipwa na madai 209 yanaendelea kufanyiwa kazi.

Kadhalika, Mhe. Jaji Mkuu alibainisha maeneo ya vipaumbele vya Mahakama ambayo ni pamoja na Kuharakisha utatuzi wa mashauri ya kawaida na mkakati wa kumaliza mashauri ya muda mrefu (backog) kwa ngazi zote za Mahakama, kuboresha mifumo ya TEHAMA kama nyenzo muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma.

Mengine ni kuimarisha ukaguzi na ufuatiliaji wa kazi za Mahakama kwa ngazi zote, kuendelea kutekeleza Mpango wa ujenzi na ukatabati wa miundombonu ya Mahakama, kushughulikia suala la maslahi ya watumishi hasa malimbikizo ya mishahara na kuwa na ngazi za mishahara ya Mahakama (Judiciary Scale) kwa watumishi wote na mengineyo.

Katika kikao hicho cha siku mbili (2) Wajumbe wa Baraza pamoja na Wawakilishi wa Wafanyakazi wa Mahakama nchini watajadili masuala mbalimbali kwa mustakabali wa Watumishi wa Mahakam ana Taasisi kwa ujumla ambapo watatoka na mapendekezo ya namna bora ya kutekeleza mambo mbalimbali yatakayoleta tija kwa Watumishi na Taasisi kwa ujumla na hatimaye huduma ya utoaji haki kuboreka zaidi.

Comments (0)

Leave a Comment