Post Details

MSAJILI MKUU AWATAKA WATUMISHI WA MAHAKAMA KUONGEZA KASI KWENYE MATUMIZI YA TEHAMA

Published By:LYDIA CHURI

 Na Mwandishi -Mahakama.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kuongeza kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hususan katika ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao.

Akikagua shughuli za Mahakama wilayani humo, Msajili Mkuu pia amewataka watumishi hao kuhuisha mara kwa mara taarifa kwenye mfumo wa kuratibu na kusajili mashauri (JSDS) ili kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za Mahakama.

Kuhusu mashauri yanayohusu masuala ya Mirathi, Msajili Mkuu amewataka Mahakimu kuhakikisha wanazingatia taratibu za ufungaji wa mashauri hayo. Aidha, Kiongozi huyo pia amewataka Mahakimu Pamoja na watumishi wengine wa Mahakama kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili na kuepukana na vitendo vinavyokiuka maadili ya utumishi.

“Mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku kwa kuzingatia maadili mtasaidia kuimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama”, alisisitiza Mhe. Chuma.

Akiwa katika ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama, Msajili Mkuu pia alipata nafasi ya kumtembela Mkuu wa wilaya ya Mvomero ambapo alimwambia kiongozi huyo kuwa upo umuhimu wa kuhakikisha upelelezi wa mashauri unafanyika kwa haraka ili mashauri yamalizike mahakamani kwa wakati.

Mhe. Chuma pia alimwomba Mkuu wa wilaya kuendelea kusimamia kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya wilaya kwa karibu zaidi kwa lengo la kuimarisha maadili.

Msajili Mkuu pia aliwaomba viongozi wa Serikali wilayani humo kutoa elimu kwa wananchi juu ya taratibu mbalimbali za Mahakama na pia kuendelea kuwaeleza kuhusu maboresho mbalimbali yanayofanywa na Mahakama.

 

Comments (0)

Leave a Comment