Post Details

JAJI KIONGOZI APONGEZA USHIRIKIANO WA MKOA WA KIGOMA KWA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzanaia, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa jitihada zake za kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania za kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi wa Mkoa huo.

Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Bw. Thobias Andengenye alipomtembelea Ofisini kwake mapema Aprili 21, 2021 Mjini Kigoma, Jaji Kiongozi Dkt. Feleshi alieleza kuridhishwa kwa jinsi Mahakama inavyopewa ushirikiano na Uongozi wa Mkoa katika masuala ya kiutendaji hasa ya kuanzishwa kwa maeneo mapya ya kiutendaji wa Mahakama.

“Natambua kuanzishwa kwa huduma ya Mahakama ya Rufani  na Mahakama Kuu katika Mkoa huu, Uongozi wa Mkoa umeshirikiana nasi kwa kiwango cha hali ya juu na hata wakati tunazindua jengo la Mahakama Kuu mwaka jana uongozi ulitoa msaada mkubwa katika kuandaa shughuli ile iliyoongozwa na Hayati Rais Magufuli hatuna budi kutoa pongezi zetu kwa Uongozi”, alieleza Jaji Kiongozi.

Aidha, Jaji Kiongozi aliongeza kuwa jukumu moja wapo la Viongozi ni kupima matokeo mathalani kwa kuanzishwa huduma ya Mahakama Kuu kwa maana ya kusimamia kwa ukaribu Mahakama za chini kama Mahakama ya Mkoa, za Wilaya na Mwanzo kumeongeza ufanisi na tija katika huduma ya utoaji wa haki.

"Kwa viwango na vigezo Mahakama ilivyojiwekea viashiria vinaonyesha matokeo ya kuanzishwa kwa huduma ya Mahakama Kuu Mkoa wa Kigoma matokeo yake yanalidhisha kwani Viongozi wa Kanda hii wamekuwa mstari wa mbele wakizunguka maeneo yote kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama ili kuwaweza kuendesha na kumudu majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi kwa wakati na kwa viwango vya kuridhisha wadau wetu," aliongeza Jaji Kiongozi.

Dkt. Feleshi alimweleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa  utendaji wa Masjala Kuu ukitoa  masjala 4 maalumu za Ardhi, Kazi, Biashara na Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi utaona hakuna Masjala yenye mlundikano wa kesi ukilinganisha na vigezo ambavyo Mahakama ilivyojiwekea vya umri wa mashauri kukaa Mahakamani ndani ya miezi 24.

Jaji kiongozi pia alitoa rai kwa Uongozi wa Mkoa na kamati nzima ya usalama inapotimiza majukumu yake itambue kuwa Mahakama inatoa huduma ya haki kwa wananchi na suala la haki ni jambo la kiusalama na linahusisha wadau wote muhimu, hivyo akaiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuendelea kusaidia kadri inavyowezekana ili kuleta utengamano katika shughuli za kiutendaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Bw. Thobias Andengenye ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa jitihada zake za makusudi kuanzisha huduma ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani Mkoani Kigoma kwani imetatua changamoto ya muda mrefu ya wananchi wa Mkoa huo kufuata huduma kwa umbali mrefu mkoani Tabora.

“Huduma hii sasa inamwezesha mwananchi kutafuta haki karibu kabisa hata kwa ngazi ya juu na ya mwisho ya kimahakama, imepunguza manung’uniko ya je? nitapata wapi nauli ya kusafiri kufuata huduma hii huko mkoani Tabora, maswali yote ya wananchi na wadau wa Mahakama yamepatiwa ufumbuzi”, aliongeza Mkuu huyo wa Mkoa.

Akielezea hali ya uendeshaji wa Vikao vya Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama Bw. Andengenye alisema kikao cha hivi karibuni cha kamati hiyo kilichokaa hakikuibua changamoto yoyote ya kiutendaji wa shughuli za Mahakama kwa kiasi kikubwa hali ni shwari  na hakukubainika changamoto ya maadili na ya kiutendaji kwa Maafisa hao.

Mkuu wa Mkoa alisema changamoto iliyopo ni ukosefu wa elimu na uelewa mdogo wa taratibu za kimahakama kwa baadhi ya wadau, hivyo wanashirikiana na Mahakama kutoa elimu kwenye maeneo hayo ili wananchi wapate uelewa katika kutafuta haki zao.

Wakati huo huo Jaji Kiongozi alipata wasaa wa kukutana na Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na kupokea taarifa ya kiutendaji na kutoa salamu za Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.  

Comments (0)

Leave a Comment