Post Details

WAJIBIKENI KATIKA MAENEO YENU YA KAZI; KABUNDUGURU

Published By:Mary C. Gwera

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru ametoa rai kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama nchini kuendelea kuwajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwa na usimamizi thabiti wa bajeti ili kufanikisha mipango mbalimbali ya Mahakama inayolenga kuboresha huduma ya utoaji haki nchini.

Akifunga rasmi Mafunzo Elekezi ya Utunzaji Kumbukumbu kwa Watendaji hao Aprili 17, 2021 katika Chuo cha Mipango jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu aliwahakikishia washiriki hao kuwa katika kutekeleza shughuli mbalimbali bajeti ya Mahakama ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 imezingatia mahitaji muhimu ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi.

“Ni matumaini yangu mtaongeza bidii na kujitoa zaidi na zaidi ili kufanikisha majukumu ya kuhakikisha kuwa huduma za Mahakama zinapatikana kwa wakati unaostahili kwa mujibu wa taratibu na viwango vinavyokubalika,” alisema Bw. Kabunduguru.

Mtendaji Mkuu aliongeza kuwa pamoja utekelezaji wa majukumu ya kimkakati aliwataka Maafisa hao wa Mahakama kuendelea pia kusimamia na kuhamasisha matumizi bora ya TEHAMA kila mmoja kwa eneo lake.

“Mahakama inatarajia kuanza utekelezaji wa mpango mkakati mpya ambapo katika mkakati huo imepanga kuongeza matumizi ya huduma za ki-elektroniki kwenye shughuli za Mahakama,” alisisitiza.

Hali kadhalika, aliwakumbusha Washiriki wa Mafunzo hayo kuendelea kusimamia miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ili kuwa na udhibiti bora wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA iliyopo Mahakamani.

Kwa upande wake, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma aliwakumbusha washiriki wa Mafunzo hayo kushirikiana katika kazi kwa kuwa wote wanajenga nyumba moja.

“Shirikianeni kutekeleza azma ya utoaji haki kwa wakati, bila kusahau kutekeleza kwa wakati maagizo yanayotolewa na Viongozi ili kusonga mbele,” alisema Mhe. Chuma.

Msajili Mkuu aliongeza kwa kuwataka Wasajili na Watendaji hao kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi walio chini yao ili kuwapa motisha ya kufanya kazi zaidi.

Katika mafunzo hayo Washiriki walipitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo uhusiano na umuhimu uliopo baina ya utunzaji kumbukumbu, matumizi ya majalada na uandishi wa nyaraka mbalimbali, usajili wa mashauri kwa mfumo wa kielektroniki.

Nyingine ni usimamizi na ukaguzi wa Mahakama, usimamizi wa masuala ya fedha na kumbukumbu zake kupitia mfumo mpya wa ‘MUSE’ na mifumo ya ndani na usimamizi wa bajeti.

Comments (0)

Leave a Comment