Post Details

SHIRIKIANENI NA MAHAKAMA ILI KUIFIKISHA KWENYE AZMA YA KUTOA HAKI KWA WAKATI: JAJI MKUU

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama, Arusha

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaomba wadau wa Mahakama kushirikiakiana na Mhimili huo ili kusaidia kuufikisha kwenye azma yake ya kutoa haki kwa wakati.

Akifungua Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau mkoani Arusha, Jaji Mkuu amesema mchango wa wadau ni nguzo muhimu katika mafanikio ya Mahakama hivyo endapo watashirikiana kwa dhati na mhimili huo watasaidia kuufikisha kwenye lengo lake kuu la utoaji wa haki kwa wakati.

“Ushirikishwaji wa wadau ni jambo muhimu na Mahakama inalizingatia hilo ili kuweza kutekeleza majukumu yake ya upatikanaji wa haki kwa urahisi”, alisema Jaji Mkuu.

Baadhi ya wadau wa Mahakama ni pamoja na Polisi, Magereza, Uhamiaji, Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mkemia Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea.

Aidha, Jaji Mkuu alisema Mahakama imesimamia nguzo tatu muhimu katika kutekeleza jukumu lake la msingi ambapo kupitia nguzo ya kwanza imeweza kujibadilisha na kufuata utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali kwani bila ya kuwa na nguzo hii shughuli za utoaji haki haziwezi kuwa endelevu.

Alisema kupitia nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wake wa miaka mitano,  Mahakama imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati. Aliongeza kuwa nguzo ya tatu ya Mpango huo ni kuimarisha imani ya wananchi kuhusu Mahakama yao na mifumo ya utoaji haki.

“Ili tuweze kutoa haki kwa wakati, imani ya wananchi ni jambo la muhimu na tunalithamini sana, wananchi ni chimbuko la mamlaka zote yaani Serikali, Bunge na Mahakama”, alisisitiza.

Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akielezea matarajio ya Mahakama kwa wadau alisema Mahakama inapenda kuona wapelelezi wakitumia njia za kisayansi katika kufanya kazi yao na kuondokana na upelelezi wa kimazoea. Alitoa mfano wa matumizi ya vipimo vya DNA katika mashauri ya jinai kwani sheria ziko vizuri katika suala hili.

Jaji Kiongozi alisema wapelelezi hawana budi kushirikiana na Mahakama ili kukamilisha upelelezi wa mashauri kwa haraka na inatarajia kuona matumizi ya adhabu mbadala kwenye makosa ya jinai mepesi ili kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani.

Aidha, Jaji Kiongozi suala la Maafisa ustawi wa jamii kuwepo mahakamani hasa kwenye mashauri yanayohusu Watoto ni muhimu na amesisitiza suala hili kwa kuwa hivi sasa halifanyiki kwa kiwango kinachotakiwa.

Kuhusu uhusiano wa Mahakama na wadau wake, Dkt. Feleshi amesema ni mzuru na hauna budi kuendelezwa. Aliongeza kuwa kwa wale wadau wasiotimiza wajibu wao ipasavyo, Mahakama itaendelea kuwaweka hadharani ili Umma na wale wanaotafuta haki wawabaini.  

Tume ya Utumishi wa Mahakama inaendelea na ziara katika Mikoa ya Arusha na Manyara kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu kwa wadau wa Mahakama wakiwemo wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya zinazowajumuisha wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.

 

  

Comments (0)

Leave a Comment