Post Details

WASAJILI NA WATENDAJI WA MAHAKAMA WAMALIZA MAFUNZO; WAAHIDI KUBORESHA UTENDAJI

Published By:Mary C. Gwera

Kundi la kwanza la baadhi ya Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania waliokuwa wakishiriki katika Mafunzo Elekezi ya Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka za Mahakama wamemaliza Mafunzo hayo ambapo wameushukuru uongozi wa Mahakama kwa kuwapatia mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo.

Akizungumza kwa niaba ya Washiriki, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya- Mhe. Projestus Kahyoza amesema kuwa mafunzo waliyopatiwa yana umuhimu katika utendaji kazi wao hivyo yatolewe mara kwa mara ili kuleta tija katika utendaji kazi

“Wasajili na Watendaji ni injini muhimu katika uendeshaji wa Mahakama, hivyo ni vyema mafunzo mbalimbali yaendelee kutolewa hadi kwa watumishi wa ngazi za chini ili kufanikisha azma ya Mahakama ya utoaji haki kwa wote na kwa wakati,” alieleza Mhe. Kahyoza.

Akifunga rasmi mafunzo hayo, Msajiliwa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina aliwapongeza Washiriki hao kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kuwataka kuendeleza ushirikiano walionao katika kutekeleza majukumu yaliyopo mbele yao.

Aidha, Mhe. Mhina aliitaka Ofisi ya Mafunzo kuongeza wigo wa mafunzo kwa ngazi zote za Mahakama ili kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo.

Kundi la pili la Washiriki wa Mafunzo linatarajiwa kuanza Mafunzo Aprili 15 hadi 17, 2021.

Comments (0)

Leave a Comment