Post Details

SIMAMIENI UTUNZAJI BORA WA KUMBUKUMBU ZA MAHAKAMA; JAJI SIYANI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Mustapher Siyani ametoa rai kwa Wasajili na Watendaji wa Mahakama kuendelea kusimamia suala la utunzaji kumbukumbu ikiwemo mifumo ya TEHAMA ambayo pia inatumika kama moja ya nyenzo za utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za Mahakama.

Akifungua rasmi Mafunzo elekezi ya siku tatu (3) kwa Wasajili na Watendaji wa Mahakama kuhusu Utunzaji bora wa kumbukumbu na Nyaraka yanayofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango-Dodoma, Mhe. Jaji Siyani alisema kuwa Mahakama ya Tanzania ni mhimili ambao umekasimiwa jukumu la kutoa haki katika nchi yetu, hivyo utunzaji kumbukumbu na nyaraka iwe za mashauri au utawala ni jambo la muhimu na lisiloepukika.

“Niwakumbushe kwamba ninyi ni viongozi, hivyo mnalo jukumu la kusimamia shughuli za Mahakama ikiwemo usimamizi wa mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu, hivyo mafanikio ya Mahakama yanategemea sana utendaji wenu kwa manufaa ya wananchi tunaowatumikia,” alieleza.

Alisema kuwa Mahakama imepiga hatua katika usanifu, ujenzi, usimikaji na usimamizi wa mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa kusajili Mashauri kwa njia ya Kielektroniki (JSDS2) yote ikiwa inalenga katika kurahisisha upatikanaji wa kumbukumbu na hatimaye huduma ya utoaji haki iweze kupatikana kwa wakati.

Hali kadhalika, Mhe. Jaji Siyani aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kupendekeza maboresho yanayoweza kufanyika katika mifumo iliyopo Mahakamani ili kutatua changamoto zilizopo.

Katika mafunzo haya yaliyoandaliwa na Mahakama kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto washiriki watapitishwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uhusiano na umuhimu uliopo baina ya utunzaji kumbukumbu.

Mengine ni matumizi ya majalada na uandishi wa nyaraka mbalimbali, usajili wa mashauri kwa mfumo wa kielektroniki, usimamizi na ukaguzi wa Mahakama, usimamizi wa masuala ya fedha na kumbukumbu zake kupitia mfumo mpya wa ‘MUSE’ na mifumo ya ndani na usimamizi wa bajeti.

Mafunzo haya yaliyofunguliwa rasmi leo Aprili 12, 2021 yanatarajia kuhitimishwa Aprili 14 mwaka huu. Aidha, kundi la pili la Wasajili na Watendaji wa Mahakama watapatiwa mafunzo kama haya kuanzia Alhamisi Aprili 15, 2021 hadi Aprili 17, 2021.

Comments (0)

Leave a Comment