Post Details

RAIS MAGUFULI AZIKWA KWAO CHATO

Published By:LYDIA CHURI

  • Rais Samia Aagiza Mchakato wa Chato kuwa Mkoa kukamilika
  • Jaji Mkuu amuelezea kuwa kiongozi aliyekuwa na ndoto za kuendeleza watanzania

Na Lydia Churi-Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kukamilika kwa mchakato wa kuifanya wilaya ya Chato kuwa mkoa na kusema kuwa endapo wilaya hiyo itakidhi vigezo vya kuwa mkoa Serikali itapitisha na isipokidhi maelekezo mengine yatatolewa.

Akizungumza katika Ibada ya Mazishi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wilayani Chato Mhe. Samia alisema Serikali itatekeleza ahadi zote zilizopo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na zile alizozitoa hayati Dkt. Magufuli kwa wananchi wake.

Mhe. Samia alisema Serikali haitawaacha wananchi wa Chato ikiwemo familia ya hayati Dkt. Magufuli. Ameishukuru familia pamoja na ofisi binafsi ya Rais kwa ushirikiano waliotoa kwa serikali katika kipindi cha msiba.

Alisema maono, mikakati na falsafa ya Hapa Kazi Tuu itaendelea kuwepo na kufanyiwa kazi. Aliwataka watumishi wa Umma na Sekta binafsi kufanya kazi kwa bidii na kuonyesha upendo na mshikamano ili kuliendeleza taifa.

“Naungana na Spika wa Bunge katika andiko la Biblia Isaya 41:10, Mungu hatatuacha, tumwelekee yeye naye atatushika mkono, tuendelee na yale tuliyopanga”, alisema Mhe. Rais.      

Rais Samia alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Mwakilishi wa wazee wa Chato Mzee Samwel Bigambo alipokuwa akitoa salaam kwa niaba ya wazee wa Chato wakati wa Ibada ya mazishi. Mzee Bigambo alikumbusha ahadi ya kuifanya wilaya ya Chato kuwa mkoa iliyotolewa wakati wa uhai wa Rais Magufuli.

Akitoa salaam katika Ibada ya mazishi, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuelezea aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuwa alikuwa ni kiongozi shupavu aliyekuwa na maono na ndoto za kuendeleza maisha ya watanzania.

Jaji Mkuu alisema Mhe. Magufuli alikuwa ni moja ya viongozi wa Afrika wenye maono ya mbali na aliyejali wananchi wake na kutetea wanyonge katika kipindi cha uongozi wake alipokuwa hai.

“Hayati Rais Magufuli alikuwa ni kiongozi aliyehoji mambo mengi ikiwa ni pamoja na kwa nini sheria na taratibu hazina kasi na matarajio ya karne ya 21” alisema Jaji Mkuu.

Alisema Mahakama ya Tanzania ni shahidi wa ndoto na maono aliyokuwa nayo hayati Dkt. John Pombe Magufuli na wapi alitaka kuipeleka nchi ya Tanzania kimaendeleo. Aliongeza kuwa mwaka 2016 alisaini mkataba wa mkopo wa shilingi bilioni 135 kutoka Benki ya Dunia uliowezesha maboresho makubwa kufanywa na Mahakama ya Tanzania.

“Historia ya Rais Magufuli bado inajiandika na haitakamilika mpaka pale miradi ya Mahakama iliyoanza itakapokamilika” alisema Jaji Mkuu wa Tanzania na kuongeza kuwa lengo lilikuwa ni kukamilisha ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo na Mahakama Kuu zote lakini anaamini kazi hiyo itakamilika chini ya uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Jaji Mkuu alisema Mahakama itampa ushirikiano unaostahili Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan na anaamini Rais huyo atatimiza ndoto alizokuwa nazo hayati Magufuli na ataifikisha Tanzania mahali inapotaka kufika kimaendeleo.

Katika hafla hiyo, Jaji Mkuu alifikisha salaam za rambirambi alizopokea kutoka kwa Majaji wakuu wa nchi kadhaa zikiwamo Rwanda, Gambia na Namibia pamoja na salaam kutoka Benki ya Dunia na Katibu Mkuu wa chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya madola.

Wakati huo huo, Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na hayati Magufuli ya kufanikisha Serikali kuhamia Dodoma katika kipindi cha miaka miwili. Alisema hayati Magufuli amefanya mambo mengi makubwa kwa maendeleo ya taifa katika kipindi cha miaka mitano pekee na kuushangaza ulimwengu.

Naye Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amepongeza kazi iliyofanywa na hayati Magufuli enzi ya uhai wake na kuiletea nchi maendeleo makubwa na hatimaye kuifikisha kwenye uchumi wa kati. 

Alisema hayati Magufuli alikuwa ni waziri wake hodari aliyeweza kumudu kufanya kazi vizuri katika wizara mbalimbali zikiwemo Ardhi, Mifugo na Uvuvi pamoja na wizara ya Ujenzi na Miundombinu. Aliongeza kuwa akiwa wizaya ya Ujenzi  alifanya kazi kubwa katika kuunganisha mikoa ya Tanzania kwa barabara za kiwango cha lami. 

Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam baada ya kuugua na kuzikwa Machi 26, 2021 nyumbani kwake Chato mkoani Geita. 

 

Comments (0)

Leave a Comment