Post Details

MAHAKAMA NA OR -TAMISEMI KUSHIRIKIANA KIMFUMO

Published By:Mary C. Gwera

Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inashirikiana na Mahakama ya Tanzania kupitia Mfumo wa Mahakama wa Kielektroniki wa Uratibu wa taarifa za Mashauri (JSDS) ili waweze kupata taarifa za mashauri za Halmashauri mbalimbali nchini.

Akizungumza katika kikao cha kubadilishana uzoefu kati ya Mahakama na OR TAMISEMI kilichofanyika Machi 26, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Kitengo cha Maboresho Mahakama (JDU), Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mahakama ya Tanzania- Mhe. Eva Nkya alisema ushirikiano huu umejikita katika eneo la Kitehama.

“Ushirikiano wetu umejikita katika eneo la Tehama ambapo, wenzetu wa TAMISEMI wamevutiwa na mfumo wetu wa JSDS hivyo wamekuja kuangalia jinsi mfumo huu unavyofanya kazi na kuona jinsi gani mfumo huu unaweza kuwekwa pia TAMISEMI,” alisema Mhe. Nkya.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Sheria, OR-TAMISEMI, Bw. Eustace Ngatale alisema kuwa andapo wataunganishwa katika Mfumo huo utawasaidia kufahamu mzigo wa mashauri yaliyopo kwa Halmashauri za Miji na za Wilaya.

“Mfumo huu pia utatuwezesha kushughulikia changamoto mbalimbali na vilevile kujua aina ya mashauri/kesi zinazokabili halmashauri mfano; mashauri ya mapato, mikataba, ardhi, watumishi na kadhalika,” alieleza Bw. Ngatale.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kupitia mfumo utawezesha kufuatilia na kufanya kazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kutimiza matakwa yote ili mashauri yasikae muda mrefu.

Katika kikao hicho Maafisa watatu kutoka OR-TAMISEMI ambao ni Mkurugenzi Msaidizi wa Sheria, Afisa Sheria Mkuu na Afisa TEHAMA walipata nafasi ya kuwasilishiwa jinsi mfumo wa JSDS unavyofanya kazi ambapo walionyesha kufurahishwa na mfumo huo.

Katika ushirikiano huu Mahakama ya Tanzania na OR TAMISEMI watajenga mfumo shirikishi utakaowazeshesha TAMISEMI kupata taarifa za mashauri yao kama ilivyoainishwa awali.

Comments (1)

  • Photo Loading... Hassan Mwalimu

    Hongereni sana kwa mashirikiano mazuri. Wananchi tunatarajia kupata huduma nzuri zaidi.

    28-03-2019

Leave a Comment