Published By: | innocent.kansha |
---|
- Namba ya bure ya mrejesho yatambulishwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro.
- Fomu maalumu za mrejesho juu ya huduma za kimahakama zakabidhiwa kwa wafungwa na mahabusu gereza la Karanga Moshi.
Na Paul Pascal-Mahakama Moshi
Watumishi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Mahakama ya Tanzania wamefanya ziara ya kikazi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi pamoja na Gereza Kuu la Karanga Moshi ikiwa ni ziara ya kuimarisha uhusiano na kuhimiza mrejesho wa huduma zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania kwa njia ya maoni, malalamiko na mapendekezo ya kuboresha huduma kwa mteja.
Akizungumza mara baada ya kuwasili ofisi ya Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Moshi mnamo tarehe 28 Oktoba, 2024 Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania Bi. evetha Mboya aliieleza historia fupi ya uanzishwaji na lengo la uanzishwaji wa kituo hicho.
“Kituo chetu cha huduma kwa wateja kilianzishwa mwaka 2022 ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2020/21 had 2024/25 akatika kutekeleza nguzo ya tatu ya urejeshaji wa imani kwa wananchi kikiwa na lengo la kuwajumuisha na kuwashirikisha wananchi kupima huduma wanazopatiwa kama zinafikia matarajio hayo. Ikilenga kuwapa wananchi fursa ya kutoa maoni, malalamiko na mapendekezo juu ya huduma za kimahakama katika eneo linalowahudumia.” alisema Bi. Mboya
Sambamba na hilo watumishi hao kutoka Kituo hicho walipata wasaha wakuzungumza na wananchi waliofika kwa ajili ya kupatiwa huduma za kimahakama katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, wajumbe huo ulifafanua huduma mbalimbali za Kituo hicho ikiwemo kuwaelekeza matumizi ya namba ya simu inayotumika kutolea mrejesho wa huduma kwa wateja pamoja na kuwaelimisha matumizi ya namba hiyo.
“Ndugu zangu kituo chetu cha huduma kwa wateja tunayo namba ya simu kwaajili ya kupokea maoni, malalamiko na mapendekezo juu ya huduma zinazotolewa na Mahakama bila kujali ni Mahakama ya ngazi ipi na iko Mkoa gani au Wilaya gani. Kituo kinapokea mrejesho wa huduma kwa Mahakama zote zilizopo Tanzania Bara kuanzia ngazi ya Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama Kuu zote kupitia namba za Bure bila malipo yoyote.” Alifafanua Bi. Mboya.
Akizitaja namba hizo za simu Mhe. Magesa Luponya alisema ni 0800750247 na whatsapp ni 0752500400. Kisha akawaomba wananchi wanapokuwa na haja ya kutoa mrejesho wowote kutumia namba hizo kwa mawasiliano na Kituo ili watumishi wa Kituo hicho kiwahudumie ipasavyo.
Ziara hiyo ya siku moja ilihitimishwa kwa wajumbe hao kutembelea Gereza Kuu la Karanga mjini Moshi nakuwapatia wafungwa na mahabusu fomu maalumu za mrejesho wa huduma za Mahakama ili kuwawezesha kutoa maoni, malalamiko na mapendekezo juu ya huduma zitolewazo na Mahakama ya Tanzania.