Published By: | innocent.kansha |
---|
Na Daniel Sichula – Mahakama Mbeya
Mahakama ya Wilaya Kyela, Kanda ya Mbeya imetoa elimu ya namna bora ya kutatua migogoro itokanayo na biashara katika maonesho ya biashara na huduma za bidhaa zinazozalishwa Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Southern International Trade Fair and Festival). Maonesho hayo yanayofanyika katika fukwe za Matema Beach wilayani Kyela yalianza tarehe 21 Oktoba na kuhitimishwa tarehe 27 Oktoba 2024.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya ikiwakilishwa na Mahakama ya Wilaya ya Kyela ikatumia jukwaa hilo kutoa elimu ya namna bora ya kutatua migogoro ya kibiashara, ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wadau juu ya shughuli mbalimbali za huduma ya utoaji haki kwa wananchi kupitia mifumo ya kidijiti na kuainisha malengo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama.
Akitoa elimu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama Wilaya ya Kyela Mhe. Andrew Severin Njau kwa kushirikiana na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kyela walijikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufunguaji, uendeshaji na utatuaji wa migogoro ya kibiashara kwenye Mahakama ya Biashara (Commercial Court) na Mahakama za kawaida.
Aidha, elimu hiyo pia iliangazia taratibu za ufunguaji na uendeshaji wa mashauri ya mirathi na utatuzi wa migogoro inayoibuka maeneo ya kazi. Hiyo kupitia maonesho hayo wadau mbalimbali walinufaika na elimu hiyo iliyotolewa na watumishi wa Mahakama lengo ikiwa ni kujenga taswira chanya na kuimarisha imani ya wadau kwa Mahakama.
Ikiwa ndiyo kwa mara ya kwanza maonyesho hayo ya kibiashara yanafanyika mkoani Mbeya, jumla ya nchi saba za Kusini mwa Afrika zimeshiriki maonesho hayo ikiwemo Rwanda, Zambia, Burundi, Malawi, Uganda, Kenya pamoja na mwenyeji Tanzania.