Published By: | Mary C. Gwera |
---|
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kampala
Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni leo tarehe 01 Oktoba, 2024 amefungua Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF) na kuhimiza ushirikiano na matumizi ya fursa zilizopo katika nchi zao ili kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Museveni amesema kuwa uwepo wa jukwaa hilo ni fursa muhimu ya kuwaunganisha na kutatua changamoto zinazowakabili kwa pamoja kama walichokifanya Marais Julius Kambarage Nyerere, Jomo Kenyatta na Milton Obote kuunganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Najua hapo katikati Jumuiya hii ilivunjika, lakini nimefanya kazi na Rais Ali Hassan Mwinyi na baadaye Rais Benjamin Mkapa na Rais Daniel Arap Moi tukaifufua na baadaye nchi za Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan ya Kusini na sasa Somalia wamejiunga,” amesema.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Jukwaa hilo, Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy-Owiny alisema kuwa Jukwaa hilo lilianzishwa mwaka 2003 kama taasisi inayowaleta pamoja Majaji Wakuu na Majaji kutoka zaidi ya nchi 50 za Ukanda huo kujadili masuala yanayohusu utoaji haki katika nchi zao.
Alieleza kuwa Mkutano huo ni fursa ya kukusanya uzoefu kutoka maeneo mbalimbali na kupitia jukwaa hilo wanakumbushwa mara kwa mara majukumu mazito yanayohitaji utayari, kujifunza kutoka kwa wenzao na kubadili fikra pale inapobidi.
"Barani Afrika, changamoto katika utoaji haki zinafanana ambazo ni pamoja na uhaba wa miundombinu ya Mahakama, ucheleweshaji unaojulikana kama mlundikano wa mashauri, vikwazo vya kijiografia, maendeleo ya kiuchumi ya kijamii, umaskini, gharama kubwa za huduma za kisheria, kutojua sheria, rushwa, mfumo mbovu wa kiteknolojia na kuingiliwa uhuru wa Mahakama.
"Kupitia kaulimbiu ya jukwaa hili inayosema, “, tunakumbushwa kuwa hatujafanya vya kutosha kuwawezesha wananchi wetu kufikia haki, jambo ambalo ni haki ya msingi ya binadamu,” alisema.
Mhe. Chigamoy-Owiny alieleza kwamba ni muhimu kwa wote kama wakuu wa Mahakama katika mamlaka zao kuhakikisha haki hiyo inalindwa na kukuzwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SEACJF na Jaji Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Mhe. Bheki Maphalala alieleza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kukuza, kulinda na kutetea uhuru wa Mahakama katika nchi za Ukanda wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Alieleza maelengo mengine ni kukuza haki za binadamu na utawala wa sheria na kuimarisha upatikanaji wa haki, kuendeleza ulinzi wa uhuru wa Mahakama na kukuza ustawi na wajibu wa Majaji katika nchi wanachama.
Mhe. Maphalala alibainisha kuwa wanatambua uhuru wa Mahakama kama unavyoainishwa katika Katiba kutoka nchi wanachama. Hata hivyo, alisema, kiuhalisia kuna utofauti katika baadhi ya maeneo ambapo Majaji wanaendelea kuingiliwa uhuru wao kwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na mikataba ya kimataifa.
Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma anaongoza ujumbe wa Mahakama kutoka Tanzania. Viongozi wengine wa Mahakama kutoka Tanzania wanaoshiriki Mkutano huo ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Leila Edith Mgonya.
Yupo pia Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kamazima Kafanabo Idd na Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim.
Ujumbe huo unajumuisha pia Mtendaji wa Mahkama Zanzibar, Bw. Kai Bashir Mbarouk, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi, Mkurugenzi wa Mipango Mahkama Zanzibar, Bw. Salum Mohamed Salum, Mkuu wa Itifaki, Bw. Juma Kapombe Mshana na watumishi wengine wawili wa Mahakama.
Ujumbe huo wa Mahakama ya Tanzania unahudhuria Mkutano huo utakaofanyika katika hoteli ya Munyonyo jijini hapa ambao umeandaliwa na Mahakama ya Uganda kwa kushirikiana na kamati maalum kutoka SEACJF.
Katika Mkutano huo kutakuwepo na mjadala mpana kuzungumzia dhana ya maboresho katika Mahakama barani Afrika ili kuimarisha upatikanaji wa haki atuzi wa migogoro barani Afrika.
Mkutano huo unawaleta pamoja Majaji Wakuu kutoka nchi mbalimbali Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika na Watalaam ili kutoa fursa kwa Mahakama na watendaji wengine wa haki kujadili kwa kina namna maboresho katika Mahakama yanavosaidia kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Wanasheria mashuhuri na wataalam wa sheria kutoka katika maeneo mbalimbali ya ukanda huo wanashiriki katika mijadala ya kina wakati wa mkutano huo.