Published By: | Mary C. Gwera |
---|
- Ateta na Watumishi wa Mahakama hizo
- Awasisitiza Mahakimu kutumia Mfumo wa Uratibu na Usimamizi wa Mashauri (e-CMS)
- Wasisitizwa kutozalisha mashauri ya mlundikano
Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Watumishi wa Mahakama za Wilaya Kigoma wamesisitizwa kutumia vema rasilimali fedha zinazopatikana katika kuboresha zaidi huduma za Mahakama kwa kuwa wananchi wanatarajia huduma nzuri na yenye viwango vya juu.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama za Wilaya tano za Kasulu, Kibondo, Buhigwe na Kakonko pamoja na Mahakama za Mwanzo akiwa katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama hizo hivi karibuni, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza alisema hatua hiyo ni katika kuhakikisha kuwa, changamoto zilizopo zinatatuliwa kwa haraka ili kuepusha kuzalisha mlundikano wa mashauri katika Kanda hiyo.
Aidha, aliwasisitiza watumishi kufanya jukumu zaidi ya moja pale wanapoona kuwa kuna upungufu wa nguvu kazi, kwakuwa itasaidia kuleta tija katika kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma mahakamani.
“Hakikisheni mnaweka mikakati thabiti ya kumaliza mashauri katika vituo vyenu maana kwa wakati huu Mahakama inapojipambanua katika maboresho ya kiteknolojia ni dhahiri sasa nasi twende kwa kasi hiyo ili tuweze kumhudumia mwananchi kwa viwango vya huduma vinavyokubalika kisheria, miongozo na taratibu za kazi bila kuacha maelekezo ya viongozi hii ndio itatupa thamani kubwa katika utendaji wetu wa kazi,” alisema Mhe. Kahyoza.
Pamoja na mengine, Jaji Kahyoza aliwapongeza Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Mahakama hizo kwa kuchapa kazi licha ya kuwa na changamoto za kimazingira na upungufu wa watumishi na vitendea kazi. Kadhalika amewapongeza kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa (2020/2021-2024/2025) unaolenga kuboresha huduma za utoaji haki.
Aidha, amewataka kudumisha mahusiano mazuri kazini kwa kupenda kituo cha kazi pamoja na kushirikiana vyema na wadau wote waliopo katika wilaya husika ili kurahisisha utoaji huduma za Mahakama.
Aliongeza kuwa, pamoja na maboresho ya Mahakama ya Tanzania ni vema wakatafuta namna ya kufufua Mahakama za Mwanzo Nyaronga na zingine katika Wilaya zote zisizofanya kazi katika maeneo yote ya Mkoa wa Kigoma kwa kuwa miji inakuwa na shughuli za kibinadamu zinakuwa, hivyo huduma za kimahakama katika maeneo hayo ni muhimu kuwepo ili kupunguza umbali uliopo baina ya Mahakama moja na Mahakama nyingine na hatimaye, kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kimahakama.
Jaji huyo aliwakumbusha pia watumishi hao kufanya kazi kwa ubunifu na weledi ili kuboresha zaidi huduma zinazotolewa na Mahakama hizo ili kuleta chachu katika utumishi na kurahisisha huduma kwa mteja wa Mahakama.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo aliwapongeza Watumishi wa Mahakama hizo kwa kazi nzuri wanazoendelea kufanya katika Mahakama zao na kuwasisitiza kuendelea hivyo pamoja na kudumisha ushirikiano wa kazi ili kuleta tija katika utendaji wa shughuli zao za kila siku katika kuwahudumia wananchi.
“Tuhakikishe hatuzalishi mashauri ya mlundikano na tusiruhusu pia wadau wa Mahakama zetu kuwa chanzo cha mashauri ya mlundikano ni vema sasa kuwashirikisha mikakati yenu mliyojiwekea ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kutekeleza shughuli zetu na hii itatuongezea heshima na picha nzuri ya Kigoma kuwa ya mfano kila wakati huko,” alisema Mhe. Tarimo.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Bw. Filbert Matotay aliwapongeza watumishi hao kwa jinsi wanavyojituma kufanya kazi na kushirikiana katika kuleta matokeo mazuri ya kazi.
“Nitashirikiana na uongozi wa Mahakama za Wilaya zote kuhakikisha changamoto za kiutendaji na za kiutumishi zinafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo katika kuzitatua ili kuendelea kuboresha na kutoa huduma nzuri kwa wananchi katika Mahakama zote Kanda ya Kigoma,” alisema Bw. Matotay.
Aidha, ameahidi kuendelea kutatua changamoto ya ikama ya watumishi kwa kutambua watumishi wenye uwezo na taaluma tofauti kusaidia maeneo yenye upungufu katika shughuli za Mahakama na kubainisha kwamba, ataendelea kuomba watumishi wapya kadri ya ajira mpya zinapopatikana.
Mhe. Kahyoza alifanya ukaguzi katika Mahakama hizo kuanzia tarehe 24-27 Septemba, 2024 lengo likiwa ni kujua hali ya utekelezaji wa majukumu sambamba na kufahamu changamoto mbalimbali zilizopo ili kuangalia namna ya kuzitatua na hatimaye kutoa huduma bora kwa wananchi.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)