Post Details

TENDENI HAKI KWA KUFUATA SHERIA, MIONGOZO NA USHAHIDI UNAOTOLEWA – JAJI KIHWELO

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha, Mahakama – Lushoto

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo amewataka Mahakimu Wakazi wapya 70 kutenda haki kwa kufuata sheria, miongozo na ushahidi unaotolewa mbele yao.

Akifungua mafunzo elekezi ya awamu ya pili kwa Mahakimu Wakazi hao, Jaji Kihwelo ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, akizungumza kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alisema Mahakimu wanapaswa kuamua kesi kwa kuzingatia sheria, ushahidi uliopo na miongozo ya kimahakama na si vinginevyo,

Aidha, Jaji Kiwhelo aliongeza kuwa hakuna uhuru usio na wajibu, na wajibu wao ni kutenda haki kwa kufuata sheria, kuamua mashauri kwa kuzingatia viapo ambavyo vinawataka kutenda haki pasipo kuangalia rangi, dini, chama, umri wala jinsia ya mtu.

“Msiamue mashauri hayo kwa chuki, huba, tetesi, hisia, kwa misukumo na mihemko mbalimbali, nendeni mkawe muarobaini wa kutoa suluhisho kwenye maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi katika Mahakama za Mwanzo”, alisisitiza Jaji Kihwelo.

Aliyaelezea maeneo hayo kuwa ni mashauri ya mirathi, mgawanyo wa mali za ndoa, matunzo na hifadhi ya watoto pia kukazia na kutimiza hukumu. Alisema wajibu wa Mahakimu ni kuwa makini na kuchukua tahadhali kubwa kwani maamuzi mabaya juu ya maeneo haya huumiza makundi maalumu yanayohusisha wototo, wajane, wagane na wazee, na pia huondoa imani ya wananchi kwa Mahakama.

Dkt. Kihwelo, aliwakumbusha Maafisa hao wa Mahakama kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu taswira ya Mahakama kama matumizi ya lugha chafu, kujigeuza Mungu watu, mavazi yasiyozingatia maadili ya kazi, ufuska, ubabaishaji, ulevi, kuchelewa kuanza Mahakama, kuingilia au kuhoji maswali wakati kesi ikiendelea kwa kiwango cha kupitiliza, kuchelewesha maamuzi na kutotoa nakala za hukumu. Mambo haya ni kinyume na maadili ya utumishi wa Mahakama.

Aliwahimiza kujinoa zaidi kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mifumo ya kielektroniki inayotumika mahakamani ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia.

“Raha ya kuwa Afisa wa Mahakama wa sasa ni pamoja na kuwa na ujuzi na uelewa wa kutosha katika matumizi ya TEHAMA. Pia kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuongeza tija na manufaa ya Mahakama na Taifa kwa ujumla.

Jaji Kihwelo aliwataka Mahakimu hao kutojitenga na wananchi na mamlaka zinazoongoza kuanzia ngazi ya mashina, Vijiji, Kata na Tarafa kwa kisingizio cha kulinda Uhuru wa Mahakama. Viongozi wa maeneo haya husika ni walinzi wa amani na pia ni wadau muhimu sana wa Mahakama.

Kuhusu suala la kutoa hukumu kwa wakati, Jaji Kihwelo amewahimiza Mahakimu hao kumaliza mashauri ndani ya muda usiozidi miezi mitatu na kuzingatia lengo la kumaliza mashauri 260 kwa mwaka. Kwa kufanya hivyo watafikia lengo la kutenda haki kwa wote na kwa wakati. Nawakumbusha kuchapa kazi zenu na kufunga majalada, kuwasilisha katika Mahakama za juu majalada yanayoitishwa ama kukatiwa rufaa.

Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma aliwakumbusha Maafisa hao kutambua nyadhifa zao na kujiepusha na vitendo vinavyoidhalilisha Mahakama na hategemei kuona Afisa wake kwa namna yoyote akitenda matendo yasiyoendana na kiapo chake.

“Tumieni mamlaka ya uhakimu pale ambapo taratibu zinaruhusu na si vinginevyo”, alisisitiza.

Naye, Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kevin Mhina aliwaasa Maafisa hao kuwa kazi ya uhakimu haina mambo mengi zingatieni haya kusikiliza kesi, kuandika mwenendo na kutoa maamuzi hivyo mkatende haki na kumaliza mashauri kwa wakati na kutoa nakala za hukumu kwa wakati.

“Tunapozungumzia suala la maadili watu wengi wanadhani ni rushwa na ulevi hata uendeshaji mbaya wa kesi pia inachukuliwa kama utovu wa maadili”, aliongeza Mhe. Mhina

Jumla ya Mahakimu Wakazi daraja la pili 70 waliapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Februari 26, 2021 Jijini Dar es salaam na kufanya idadi ya Mahakimu Wakazi  wapya  kufikia 140 walioapishwa katika kipindi cha wiki moja.

 

 

Comments (0)

Leave a Comment