Published By: | Mary C. Gwera |
---|
• Jaji Mfawidhi Bukoba azindua Jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili
Na AHMED MBILINYI, Mahakama-Bukoba
Huduma ya utoaji haki kwa wananchi inazidi kusogezwa karibu zaidi na wananchi, hivi karibuni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi alizindua jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili iliyopo Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
Uzinduzi wa Mahakama hiyo utawarahisishia wakazi wa Kijiji cha Nyakibimbili waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa 12 kupata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Ibwera na umbali wa Kilometa 20 kupata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Katoro.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Banzi alionesha furaha isiyo ya kifani kwa wananchi wa Kijiji hicho na majirani zake kwa kupata jengo zuri na la kisasa.
“Ikumbukwe kwamba kabla ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili, wananchi walilazimika kusafiri umbali wa kilometa 12 kupata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Ibwera na umbali wa Kilometa 20 kupata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Katoro, kwahiyo upatikanaji wa jengo hili utawapunguzia aza waliyokuwa wakiipata,” alisema Mhe. Banzi.
Jaji Mfawidhi huyo aliongeza kuwa, umbali wa hapo awali wa kufuata huduma ya Mahakama ulikuwa mrefu na wananchi waliathirika kwa kutumia muda wao mwingi kutafuta huduma za Mahakama, muda ambao wangeutumia katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Aidha, Mhe. Banzi alitumia fursa hiyo, kuwaomba wananchi kutumia Mhimili wa Mahakama kupata haki zao badala ya kwenda kwenye Mahakama zisizo rasmi ambapo alisisitiza kwa kueleza, “kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 107A, Mahakama ndio Taasisi pekee iliyopewa jukumu la kutoa haki.”
Awali, Mhe. Banzi alitembelea Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Nyakibimbili na kusalimiana na Afisa Mtendaji Kata hiyo, Bw. Bashiru Mussa.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Afisa Tawala Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, Bw. Mushobozi Nsangila alisema Mradi huo ulianza tarehe 19 Machi, 2021 na kukamilika tarehe 28 Februari, 2023.
Bw. Nsangila alisema kuwa, Mradi ulitekelezwa na Mkandarasi kutoka Kampuni ya Silva ‘Investments Limited’ na Mshauri Elekezi alikuwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Alibainisha kuwa, jengo hilo lilianza kutumika tangu mwezi wa Aprili, 2023. Na kwamba kuanza kutumika kwa jengo hilo kumeboresha utoaji huduma za kimahakama na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)