Post Details

MAJAJI WASTAAFU WATANO WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA WAAGWA KITAALUMA

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, amesema Mahakama itaendelea kuwatumia Majaji wastaafu katika shughuli mbalimbali za Mahakama nchini.

Akizungumza na Vyombo vya habari mara baada ya hafla ya kuwaaga rasmi kitaaluma jumla ya Majaji watano wa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyofanyika Machi 15 Mahakama Kuu Dar es Salaam, Mhe.Jaji Kiongozi alisema kuwa Mahakama inafanya kazi kwa karibu na Majaji wastaafu kwa kuwashirikisha katika  shughuli mbali mbali za mahakama ikiwa ni pamoja na  eneo la Mafunzo.

“Mahakama inafanya kazi kwa karibu na Majaji Wastaafu, tunashirikiana na katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la Mafunzo ambapo tunawatumia katika kutoa mada kutokana na uzoefu walio nao,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Jaji, Dkt. Feleshi alisema  kuwa mpaka sasa kuna jumla Majaji wastaafu sabini (70) , hivyo kwa kushirikiana na Majaji waliopo kazini, Mahakama inaendelea kuwatumia katika shughuli kadhaa kupitia Chama cha Majaji Wastaafu.

 Akizungumzia umuhimu wa hafla hiyo, Mhe.Jaji kiongozi amesema kuwa lengo kubwa la hafla hizi ni kuwakumbusha Wahe. Majaji waliobaki umuhimu wa wao kufanya kazi zao kwa uadilifu na ufanisi ili waweze kumaliza vizuri vipindi vyao vya uongozi kwa muda wote wa utumishi wao.

Majaji Wastaafu walioagwa katika hafla hiyo ni Mhe. Jaji Fredrica William Mgaya, Mhe. Jaji Aisha Charles Nyerere, Mhe. Jaji Rose Aggrey Temba, Mhe. Jaji Crecensia Makuru na Mhe. Jaji Salima Chikoyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Majaji hao Wastaafu wamewaasa Watumishi wa Mahakama waliobaki kufanya kazi kwa uadilifu na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Naye, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bi. Fatma Karume aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa wanawake katika sekta ya sheria huku akionesha furaha yake kwa Majaji hao wastaafu ambao wote ni wanawake.

“Nilipoanza kufanya kazi za Uwakili, miaka takribani 30 iliyopita, Sekta ya sheria ilikuwa inaendeshwa na idadi kubwa ya wanaume ukilinganisha na miaka ya hivi karibuni ambapo wanawake wamepewa nafasi katika sekta hii,” alisisitiza Bi. Karume.

Kabla ya kustaafu kwake Mhe. Jaji Mgaya alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, naye Mhe. Jaji Nyerere alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

Mhe. Jaji Teemba alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Jaji Makuru alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi naye Mhe. Jaji Chikoyo alikuwa Jaji wa Mahakama, Kitengo cha Usuluhishi.

Majaji wote wastaafu waliitumikia Mahakama na Taifa kwa ujumla katika nafasi mbalimbali za Kiutumishi.

Comments (0)

Leave a Comment