Published By: | Mary C. Gwera |
---|
Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Rai imetolewa kwa Wakandarasi pamoja na Mshauri Mwelekezi wa Ujenzi kuhakikisha wanatekeleza makubaliano ya mkataba wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo tatu ambazo ni Kigoma Kaskazini, Manyovu na Heru Juu ziweze kukamilika kwa wakati.
Akizungumza na Wakandarasi hao hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile alisema ni vema Wakandarasi hao watekeleze ipasavyo ratiba za ujenzi wa Mahakama hizo.
“Kutekeleza makubaliano haya kutaleta ufanisi katika Miradi hiyo na italeta maana kubwa kwa wananchi kupata huduma za Mahakama kwa wakati na katika mazingira mazuri yanayomrahisishia mtumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa ufanisi na kuharakisha huduma kwa wananchi,” alisema Mhe. Rwizile.
Jaji Mfawidhi huyo aliongeza kuwa, ujenzi wa Mahakama hizo ni muendelezo wa maboresho ya kusogeza huduma karibu na wananchi.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay alisema atashirikiana na Wakandarasi pamoja na Viongozi wa Mahakama za Wilaya husika kuhakikisha kuwa, ujenzi unakwenda kwa kasi na kumalizika kwa muda uliopangwa na kwa viwango vya ujenzi unaokubalika na Mahakama ya Tanzania ili kuutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama (2023/2024-2024/2025) unaoelekeza kusogeza huduma kwa wananchi na kutoa haki kwa wakati.
Naye Mkadiriaji wa Majengo, Bw. Deogratius Lukanso akitoa taarifa kwa Jaji Mfawidhi, alisema Miradi yote mitatu itakwenda kwa pamoja na itadumu ndani ya miezi sita kuanzia tarehe 01 Agosti, 2024.
Bw. Lukanso alisema kwamba, Wakandarasi hao wamepewa siku 14 ya kufanya maandalizi ya vifaa vya ujenzi pamoja rasilimali watu katika ujenzi huo utakaokamilika Februari, 2025 na itakabidhiwa Mahakama kwa ajili ya kuanza kutoa huduma za haki.
Kwa upande wake Mshauri Mwelekezi, Bw. Elibariki Shempemba alisisitiza kuwa, Mkandarasi azingatie kutoa fursa kwa wananchi kupata kazi katika Miradi hiyo, sambamba na kuzingatia afya ya watu wanaolizunguka eneo la Miradi yote mitatu, kwakuwa italeta ushirikiano baina ya Wakandarasi na wananchi wa Vijiji hivyo watakaotoa huduma mbalimbali ikiwemo Mama Lishe.
Aidha, Wakandarasi hao walisisitizwa pia kuzingatia utunzaji wa mazingira na usalama wa watu wanaozunguka eneo la Miradi yote.
Shughuli ya makabidhiano wa viwanja hivyo ilishuhudiwa na Viongozi wa Vijiji hivyo zinapojengwa Mahakama hizo. Viongozi wengine wa Mahakama walioshiriki ni Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Rose Kangwa, Mhandisi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Peter Mrosso na Mkadiriaji Majengo Bw. Deogratius Lukansola Mahakama Makao Makuu.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)