Post Details

MAHAKAMA WILAYA KIBAHA YAPONGEZA USHIRIKIANO WA WADAU

Published By:Mary C. Gwera

  • Yasema umesaidia kumaliza mlundikano wa mashauri
Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani
 
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai amewapongeza wadau wa haki jinai kwa kushirikiana na Mahakama hiyo na kuwezesha kumaliza mlundikano wa mashauri.
 
Mhe. Lukumai ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Juni, 2024 katika kikao cha kusukuma mashauri ya madai ambacho amekiongoza yeye Mwenyekiti.
 
“Kama tulivyokubaliana kuwa, ifikapo Aprili, 2024 mashauri yote yanayoonekana yanakaribia kwenye mlundikano yawe yameisha na kweli imekuwa hivyo tujipongeze wote kwa hatua hii maana azimio letu limetimia,” amesema Mhe. Lukumai.
 
Amewaomba upande wa Mashtaka na Polisi kukubaliana kuwa na maahirisho mafupi na kuongeza kuwa, sasa hivi tuko katika mtandao hivyo hata wito kwa mashahidi (summons) zitumwe tu kwa njia ya mtandao.
 
Kadhalika Mfawidhi huyo, amewataka Mawakili wa Kujitegemea kuangalia shajara zao ili kuepuka kuchelewesha mashauri ambapo amesema kwamba, mashauri mengi yenye uwakilishi wa Mawakili mara nyingi yamekuwa yakichelewa kutokana na udhuru wa Mawakili kwa kutokupanga vizuri shajara zao.
 
Naye, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Mhe. Felister Ng’hwelo amesema mashauri mengi ya Mawakili huwa na ucheleweshaji, ambapo amebainisha kuwa, wengi wao hawana sababu za msingi za kuahirisha mashauri hayo. 
 
Akitoa mfano, Mhe. Ng’hwelo amesema kwamba, alikuwa na shauri moja lenye Wakili ambaye hakutokea mahakamani kwa mara mbili na alituma Mwakilishi naye hakuwa na maelekezo ya kuendelea na shauri hilo, kufuatia hali hiyo, alifuta shuri hilo kwa kuwa hakukuwa na sababu za msingi za ucheleweshaji. Hivyo, wamemuomba Mwakilishi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Pwani, Rita Ntagazwa awafikishie taarifa hiyo ili wafuate taratibu.
 
 Akijibu hoja hiyo, Wakili Ntagazwa amesema Wakili anayetoa udhuru kuwa yuko Mahakama alete uthibitisho wa wito (summons) au ‘causelist’, lakini pia amewaomba Mahakimu pia kutokulazimisha tarehe ambayo Wakili anasema ana shauri mahali pengine na kusema kuwa, itasaidia kuondokana na usumbufu wa kutofika mahakamani wakati mashaidi wameshafika.
 
Naye Wakili wa Serikali, Dorice Kawonga amewaomba Ustawi wa Jamii kuongeza watu wanaoshughulikia masuala ya watoto maana katika Mahakama ya Wilaya na Hakimu Mkazi Pwani mpaka sasa anayetegemewa katika masuala hayo ni mmoja pekee.
 
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Mhe. Joseph Luoga amewaomba wadau wa haki jinai kuipa thamani sawa  Mahakama ya Mwanzo kama  Mahakama zingine  maana ndio Mahakama ya wananchi wa kawaida  na inabeba asilimia 70 ya wananchi ukilinganisha na ngazi nyingine za juu na ndio maana Bunge likaona ni vema kufanya marekebisho ya Sheria na kuruhusu Mawakaili kuwawakilisha wateja wao katika Mahakama hiyo. 
 
Mhe. Lukumai amewaomba Wadau hao kuendeleza ushirikiano uliopo pamoja na kutekeleza kwa pamoja yote waliokubaliana ili haki ipatikane kwa wakati.
 
Katika kikao kilichopita maazimio yaliyofikiwa ambayo ni pamoja na kushauri zaidi wadaawa kufanya usuluhishi badala ya kusikiliza mashauri na kuwaelekeza Mawakili wa Kujitegemea kufuata utaratibu wa kisheria pindi wanapokuwa Mahakama za Mwanzo yote yametekelezwa.
 

Comments (0)

Leave a Comment