Post Details

JAJI MKEHA :TOENI TUZO ZINAZOTEKELEZEKA

Published By:magreth.kinabo

Na Naomi Kitonka-Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara,Mhe.Cyprian Mkeha ametoa raia kwa mahakimu kutoa tuzo zinazotekelezeka ili kurahishisha utekelezaji wa hukumu na amri za mahakama.

 

Mhe.Mkeha alisema hayo tarehe 15 Juni, 2024 wakati akitoa mafunzo ya kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa hukumu na amri za mahakama kwa mahakimu hao wa ngazi mbalimbali kwenye ukumbi wa mafunzo wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke,kilichopo jijini Dar es Salaam.

“Lengo la utekelezaji wa hukumu siyo kumdhalilisha mdaiwa, bali ni kumwezesha mshindi wa tuzo kupata haki yake anayostahili kuipata, aliyopewa na Mahakama.” alisema Jaji Mkeha.

 

Aliongeza kwamba mahakimu hao, wanapaswa kufanya utambuzi wa mali za mdaiwa ili kuweza kubaini uwezo wake kabla ya kutoa hukumu na amri za mahakama ili kuzifanya ziweze kutekelezeka.

“Ni lazima maombi mahususi yatumwe mahakamani ili mchakatowa utekelezaji wa hukumu ukamilike,ambapo maombi hayo yanawezwa kufanya na wakili,mshindi wa tuzo au mtu aliyehamishiwa tuzo, ambapo utambuzi wa mali ni muhimu ili kuweza kupunguza mganganyiko,” alisisitiza.

Awali akifungua mafunzo hayo Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC), Temeke Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa alisema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuwajengea uwezo mahakimu hao, kwa ubadilishana uzoefu.

Akifunga mafunzo hayo,Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale alimpongeza Jaji Mkeha kwa mafunzo aliyoyatoa kwa kuwa yamesaidia kuwajengea uwezo mahakimu hao. Huku akiwataka mahakimu hao kwenda kutoa elimu waliyoipata kwa wengine.

 

“Uwezo mliojengewa ukaonekane kwenye hukumu zenu,’’ alisema Mhe. Jaji Ngunyale.

Mafunzo hayo yamewashirikisha Majaji wa Kituo hicho, Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi na Mahakimu Wafawidhi

Comments (0)

Leave a Comment