Post Details

MSAJILI MKUU AWAFUNDA WATUMISHI WA KITUO CHA HUDUMA KWA MTEJA

Published By:magreth.kinabo

  Na Mwandishi Wetu

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, jana tarehe 6 Juni, 2024, alikutana na kuzungumza na watumishi 11 Kituo cha Huduma kwa Mteja wakiwemo Mahakimu Wakazi saba ambao wamejiunga na kituo hicho hivi karibuni.

Akizungumza na Mahakimu hao, Msajili Mkuu huyo amewapongeza kwa kuteuliwa kujiunga na kituo hicho ili kuwahudumia wananchi kwa njia ya kupokea mirejesho mbalimbali kutoka kwao.

“Kituo cha Huduma kwa Mteja kimebeba taswira nzima ya Mahakama, tuna imani kubwa nanyi kwamba mtafanya kazi kwa weledi mkubwa, uadilifu pamoja na uwajibikaji kama ilivyo kauli mbiu ya mahakama…Wananchi wengi wanakuja kwenu wakiwa wamekata tamaa hivyo mnapowahudumia zingatieni weledi na lugha ya kujali wateja hao,” alisema Mhe.Msajili Mkuu Nkya.

Aidha, Mhe.Nkya aliwataka watumishi wa kituo hicho kuongeza ubunifu wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) katika kuwahudumia wateja ili kurahisisha na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma.

Akiwaasa juu ya utendaji kazi wa kila siku, aliwaambia kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu sambamba na kufanya tafiti mbalimbali zitazowezesha Mahakama kufanya maboresho kupitia mirejesho inayotolewa na wateja.

Nao viongozi wa kituo hicho Bi. Evetha Mboya (Team Leader) na Mhe. Denice Mlashani (Technical Supervisor na Hakimu Mkazi Mwandamizi) kwa niaba ya watumishi wa kituo hicho, walimshukuru Mhe.Msajili Mkuu kwa kukutana na watumishi wa kituo hicho na kuwapa nasaha muhimu ambazo zitakuwa dira katika utendaji kazi wao.

Viongozi hao, pia walimuahidi kuwa watafanya kazi kwa bidii huku wakizingatia maelekezo yote aliyowapatia.

 

Comments (0)

Leave a Comment