Published By: | LYDIA CHURI |
---|
Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha Mhe. Joachim Tiganga ametoa rai kwa Maafisa Tarafa kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na wilaya ili wazitumie kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Mahakimu.
Akifungua Mafunzo Maalum ya siku mbili kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Arusha leo Tarehe 6 Juni, 2024 jijini humo, Jaji Tiganga alisema Mafunzo hayo yameandaliwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa lengo la kuwaelimisha Maafisa hao ili nao wakawaelimishe wananchi.
”Elimu mtakayoipata mkaitumie kuwaelimisha walio chini yenu wakiwemo Watendaji wa Kata, Mitaa, Vijiji na wanachi kwa ujumla kupitia fursa mlizonazo mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku kwa wananchi”, alisema.
Alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama imeamua kuwatumia Maafisa Tarafa kuwaelimisha Wananchi kwa kuwa wao ni kiungo kati ya Serikali na wananchi katika Tarafa na pia ni wawakilishi wa wakuu wa wilaya katika shughuli mbalimbali za kijamii, miradi ya maendeleo na katika kutatua migogoro ya wananchi.
”Mafunzo haya ni moja ya utekelezaji wa misingi ya Utawala Bora ya Tume unaozingatia Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo katika usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Maadili za Mkoa na wilaya”, alisema.
Alisema ni matarajio ya Tume kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa ili wakaisaidie Tume katika kuwaelimisha wananchi namna ya kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Mahakimu.
Mafunzo kwa Maafisa Tarafa yamehusisha mada tatu ambazo ni Muundo na Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, Kanuni za Maadili ya Maafisa Mahakama na Uwasilishaji wa malalamiko na Mgawanyo wa majukumu kati ya Mihimili ya Dola.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.