Post Details

JAJI NDUNGURU AFUNGA MAFUNZO YA MAAFISA MAHAKAMA MBEYA

Published By:innocent.kansha

Na Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru amewataka Mahakimu kuwa mabalozi wazuri katika suala zima la kuponesha majeraha ya kisaikolojia kwa waathirika wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

Ameyasema hayo jana tarehe 5 Juni, 2024 wakati akifunga mafunzo yahusuyo kuepuka kutonesha majeraha ya kisaikolojia kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Mbeya yaliyojumuisha Mahakimu 15 wa ngazi mbalimbali katika Kanda ya Mbeya.

Mhe. Ndunguru amewataka Mahakimu hao kuhakikisha wanaongeza umakini katika mashauri yanayohusisha watoto na watu wengine wa makundi maalum na akatoa rai kwa washiriki hao wahakikishe wanakwenda kutoa elimu waliyoipata kwa watu wengine katika vituo vyao ili kuepuka makosa ya kutonesha majeraha kwa waathirika kutokea.

“Natoa wito kwa kila mmoja wenu kuhakikisha anakua balozi mzuri wa kuponesha majeraha kwa waathirika na sio kuwa sababu ya kuwatonesha majeraha yao. Hivyo nyote mliopata mafunzo haya mkahakikishe na wenzenu ambao hawajapata mafunzo haya wanayapata,” alisisitiza Jaji Ndunguru

Aidha, Mhe. Ndunguru aliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Irish Rule of Law International (IRLI) kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo mkoani Mbeya.

Vilevile, aliwashukuru wawezeshaji ambao waliwasilisha mada zao kwa umahiri mkubwa wakiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa na Naibu msajili kutoka Masjala Kuu Dodoma Mhe. Mvungi kwa namna walivyokuwa na utayari na kujitoa bila kuzingatia ugumu wa ratiba walizonazo, alikadhalika aliwapongeza washiriki wote wa mafunzo hayo.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe Mhe. Hassan Ahmed Makube akiongea kwa niaba ya washiriki alitoa shukrani kwa kupata mafunzo hayo na kuahidi kuwa wote kwa pamoja wanakwenda kuwa mabalozi wazuri wa mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yalifungwa kwa washiriki wote kutunukiwa vyeti vya ushiriki kutoka kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani (T) na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) kwa washiriki na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru.

Comments (0)

Leave a Comment