Post Details

KIKAO CHA BARAZA KUU WAFANYAKAZI MAHAKAMA YA TANZANIA 2024 CHAHITIMISHWA

Published By:innocent.kansha

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kilichokuwa kinafanyika kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini hapa kimehitimishwa leo tarehe 17 Mei, 2024 na Jaji Amiri wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, ambaye alikuwa Mwenyekiti akimwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha, Mhe. Mwarija amesema kuwa kumekuwa na kikao chenye mafanikio makubwa ambacho kimewawezesha wajumbe kupitia na kujadili ajenda mbalimbali zenye lengo la kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.

“Tumepata taarifa mbalimbali za utekelezaji wa kazi, tumejadili mada kuhusu miradi inayoendelea kutekelezwa kwa madhumuni ya kuboresha utendaji kazi kama vile miradi ya ujenzi, ujenzi wa TEHAMA na tumepata mada kuhusu ujasiliamali na itifaki kuhusu Viongozi na Wafanyakazi,” amesema.

Mweyekiti amebainisha pia kuwa wakati wa kikao, wajumbe wamepata nafasi ya kupitia muhtasali wa yale ambayo yalitokea katika kikao kilichopita cha tarehe 18 na 18 Mei, 2023 na kupokea taarifa mbalimbali kutoka kwa Msajili Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama.

Ameeleza pia kuwa Baraza limepata taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Mahakama kwa mwaka 2023/2024 na hali ya utekelezaji wa mifumo ya TEHAMA katika uendeshaji wa Mahakama Mtandao.

“Katika mkutano uliopita, Baraza lilipata hoja mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi wa kila kada. Jambo la kufurahisha na tumeelezwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE kuwa njia iliyotumika kutatua matatizo yaliyokuwa yamewasilishwa ilikuwa ya mafanikio ikihusisha TUGHE na Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama. Hii ni hatua nzuri,” amesema.

Mwenyekiti amebainisha kuwa katika kikao hiki, Baraza limejifunza na kuona uwepo wa mafanikio mengi, mojawapo ni ile ya utendaji wa kazi ambao katika eneo la usimamizi wa mashauri watumishi wa Mahakama wamefanikiwa kwa asilimia 100.

Wakati wa kuhitimisha kikao hicho, Mahakama ya Tanzania imemtangaza Mfanyakazi Bora wa Mhimili kwa mwaka 2024 kutoka Kanda ya Mwanza, Bw, Steven Kapiga, ambaye ni Msaidizi wa Kumbukumbu kwa kuibuka mshindi baada kuchuana na watumishi wengine wa Mahakama.

Bw. Kapiga ameibuka mshindi kutokana na utundu wake kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo kusaidia katika Mfumo wa Usimamizi na Uratibu wa Mashauri na Mfumo Mpya wa Tafsiri na Unukuzi, japo yeye hajasomea masuala ya teknolojia.

Bw. Kapinga amelieleza Baraza kuwa kufuatia utundu wake katika masuala ya TEHAMA amefanikiwa kubuni sanduku la kielekroniki la maoni linalowawezesha wananchi kutoa maoni yao kwa njia ya kielektroniki.

Mwenyekiti wa Kikao cha Baraza amemkabidhi zawadi ya cheti Bw. Kapiga kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania kwa kutambua utumishi wake uliotukuka. Bw. Kapiga ameshukuru Viongozi wa ngazi zote kwa ushirikiano anaoupata unaomwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Comments (0)

Leave a Comment