Post Details

MAHAKAMA YANG’ARA KATI YA IDARA ZA SERIKALI

Published By:innocent.kansha

Yashika nafasi ya kwanza kwenye usimamizi rasilimaliwatu 

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kupata tuzo ya mshindi wa kwanza katika Usimamizi wa Rasilimaliwatu kati ya Idara za Serikali zinazojitegemea nchini Tanzania.

Akizungumza kwenye Baraza la Wafanyakazi linalofanyika jijini hapa leo tarehe 16 Mei, 2024, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa hatua hiyo imetokana na usimamizi bora wa rasilimaliwatu.

“Tuzo hii imetolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Kikao cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu kilichofanyika Jijini Arusha, Septemba, 2023,” amesema.

Mtendaji Mkuu amempongeza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Bi. Beatrice Patrick kwa uongozi bora na watumishi wote wa Mahakama kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ambao umechangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa Tuzo hiyo.

Amewaeleza wajumbe wa Baraza kuwa katika mwaka 2023/24 Mahakama imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kwamba licha ya changamoto mbalimbali zilizopo, Watumishi wameendelea kujituma na kufanya kazi kwa weledi na hivyo kufanikisha malengo yaliyowekwa. 

“Ofisi ya Mtendaji Mkuu itaendelea kufanya kazi kwa karibu na mamlaka husika ili kuweza kutimiza azma ya kuboresha masilahi na mazingira ya kazi kwa watumishi wa Mahakama,” amesema.

Prof. Ole Gabriel ametumia fursa hiyo kuwasilisha taarifa yake kwenye Baraza hilo na kubainisha kuwa Mahakama ya Tanzania imekuwa katika mstari wa mbele kuwaendeleza watumishi ili kuboresha utendaji wa kazi.

Kwa upande wa mafunzo ya muda mfupi kwa gharama za mwajiri, Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa zaidi ya Shilingi za Kitanzania 4.2 bilioni zimetumika kugharamia mafunzo ya Watumishi na Wadau wa Mahakama 2,635. 

“Idadi hii inajumuisha watumishi 1,785 wa kada za Wasaidizi wa Kumbukumbu na Waandishi Waendesha Ofisi waliohudhuria mafunzo ya ujuzi ya kidigitali. Mafunzo haya pekee yalitumia kiasi cha zaidi ya Tsh. 2.5 bilioni,” amesema.  

Kuhusu mafunzo ya muda mrefu kwa gharama za Mwajiri, Prof. Ole Gabriel amewaambia wajumbe wa Baraza kuwa Watumishi 142 wapo masomoni na kati yao 121 wanagharamiwa na Mwajiri kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania 766,547,043/-.

Mtendaji Mkuu amebainisha pia kuwa mpaka kufikia mwezi Mei, 2024 wamepokea maombi ya watumishi 469 kujiunga na masomo kwa mwaka 2024/2025.

Akizungumzia miradi ya miundombinu ya majengo inayotekelezwa kwa mwaka 2023/2024, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa miradi 137 inatekelezwa katika ngazi mbalimbali za Mahakama.

Amesema kuwa miradi iliyokamilika hadi kufikia Aprili, 2024 kwa upande wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama za Wilaya ni Ubungo, Ulanga (Mahenge), Liwale, Kwimba na Maswa. Aidha, Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa Mahakama imekwisha pokea majengo ya Mahakama za Wilaya ya Kwimba na Maswa ambapo shughuli za kimhakama zinaendelea.

“Ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama za Mwanzo Kinesi (Rorya), Kabanga (Ngara), Madale (Kinondoni), Newala (Mtwara) na Mang’ula (Morogoro) zimekamilika na ziko kwenye hatua za mwisho za kukabidhiwa jengo,” amesema.

Aidha, Prof. Ole Gabriel amebainisha kuwa Mahakama imekwisha pokea majengo ya Mahakama za mwanzo Mahenge (Kilolo), Luilo (Ludewa) na Usevya (Mlele) ambapo shughuli za kimhakama zinaendelea.

Kuhusu miradi inayoendelea hadi Kufikia Arpili, 2024 kwenye uboreshaji wa huduma za Mahakama, Mtendaji Mkuu amesema Wakandarasi wa majengo nane ya Vituo Jumuishi vya Njombe, Songea, Songwe, Katavi, Singida, Simiyu na Geita ipo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi.

Amesema kuwa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Pemba utaanza tarehe 23 May, 2024 baada ya Mkandarasi kusaini na kukabidhiwa eneo la mradi na kwamba maandalizi ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 60 yanaendelea.

Prof. Ole Gabriel ameeleza pia kuwa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Korogwe unaendelea na kwa sasa umefikia asilimia 64 na kwamba kwa mwaka wa fedha 2024/25, Mahakama inategemea kutekeleza miradi ya Mahakama za Wilaya Handeni, Igunga, Mlele, Lushoto, Kiteto na Rufuji.    

“Miradi ya majengo ya Mahakama ya Wilaya za Kishapu, Ukerewe, Tarime, Biharamulo, Momba, Kalambo, Kilosa, Nyasa, Masasi, Chamwino, Uyui, Mkalama na Ukerewe iko kwenye hatua za manunuzi kwa ajili ya kupata wakandarasi ili kazi zianze,” amesema.

Comments (0)

Leave a Comment