Post Details

DC NASSARI KUWAELIMISHA WANANCHI UWEPO WA KAMATI ZA MAADILI YA MAHAKIMU • Yumo pia Mkuu wa Wilaya ya

Published By:LYDIA CHURI

  • Yumo pia Mkuu wa Wilaya ya Kwimba

Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Magu Mwanza

Mkuu wa Wilaya ya Magu na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilayani humo Mhe. Joshua Nassari ameahidi kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati hizo ili waweze kuzitumia katika kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa Maadili kwa Mahakimu.

Akizungumza wakati wa Utoaji wa Elimu kuhusu uwepo wa Kamati hizo inayotolewa na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama jana wilayani Magu, Mkuu huyo wa wilaya pia amewashauri wakuu wa wilaya wengine kufanya hivyo ili kuziimarisha Kamati hizo na kuwasaidia wananchi kupata haki.

’’Sisi Wakuu wa wilaya ndiyo Wenyeviti wa Kamati za Maadili na kwa kuwa kazi zetu nyingi zinatukutanisha na wananchi, nitatumia nafasi hizo kuwaelimisha wananchi wetu ili wafahamu juu ya uwepo wa kamati hizi na kuzitumia” , alisema.

Alisema ushirikiano kati ya Wajumbe wa Kamati hizo utasaidia na kuziwezesha kutekeleza jukumu lake la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama kwa urahisi na kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kwimba Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija amesema Kamati ya Maadili wilayani Kwimba imekuwa ikishirikiana na Mahakama kwa karibu na hivyo kupunguza mashauri ya kinidhamu.

Hata hivyo ameishauri Mahakama ya Tanzania kuwakumbusha Watumishi wasio Maafisa Mahakama kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na kutoingilia kazi za Mahakimu. Alisema wakati mwingine makosa ya ukiukwaji wa maadili hufanywa na watumishi hao na lawama kuelekezwa kwa Mahakimu na hivyo kuchafua taswira ya Mhimili wa Mahakama.

Kuhusu Elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili, Mkuu huyo wa wilaya ameishauri Tume kutenga fedha kwa ajili ya Watumishi wa Sekretariet ya Tume  kupita kwenye maeneo mbalimbali nchini na kutoa elimu kwa kuwa wajumbe wa Kamati hizo wamekua wakibadilika mara kwa mara.

Naye Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya alisema Tume imeandaa Kanuni na Miongozo ya Uendeshaji wa Kamati hizo kwa lengo la kuwarahisishia wajumbe wa Kamati kutekeleza jukumu lao la usimamizi wa Maadili.

Watumishi wa Sekratariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na kazi ya utoaji wa Elimu kwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya katika mikoa ya Mwanza na Mara pamoja na wilaya zake.

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment