Post Details

MAJAJI WANAWAKE UKANDA WA AFRIKA WAKUMBUSHWA KUSIMAMIA HAKI

Published By:Mary C. Gwera

Na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania-Accra, Ghana

Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. Nana Addo Dankwa Akufo-Addo ametoa rai kwa Majaji Wanawake wa Ukanda wa Afrika kutoa maamuzi yanayoakisi usawa na haki kwa jamii na utawala wa sheria.

Akizungumza leo tarehe 13 Mei, 2024 wakati akifungua Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Ukanda wa Afrika katika Hoteli ya Labadi jijini Accra, Mhe. Akufo-Addo amesema suala hilo ni muhimu kwa kuwa wana uwezo na mamlaka ya kuhakikisha mila potofu zinaondoka kulingana na maamuzi yao.

“Sauti zenu kupitia maamuzi mnayotoa zinaweza kubadilisha mila, desturi na tamaduni hasi ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, ndoa za utotoni, biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu, ukeketaji na kadhalika,” amesema Rais huyo.

Kadhalika, amewasihi Majaji hao kuifanyia kazi kaulimbiu ya Mkutano huo isemayo; Nafasi ya Majaji Wanawake katika kupambana na mila potofu katika ulimwengu wa sasa’ kwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu vitendo mbalimbali vinavyoakisi mila potofu.

Amesema kuwa, Serikali ya Ghana inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa Utawala wa Sheria unazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watu wanapata haki na si tu kupata haki bali haki kuonekana imepatikana.

“Kipaumbele chetu kama Serikali kimejikita katika kuhakikisha kuwa, kuna Utawala wa Sheria, hivyo ninaomba kila mmoja kuwajibika kuhakikisha kuwa Utawala wa sheria unazingatiwa,” amesema Rais Akufo-Addo.

Amesema, Serikali yake inaendelea na juhudi za kuboresha mazingira wezeshi ya utoaji haki ikiwa ni pamoja na kujenga Majengo ya kisasa ya Mahakama.

Naye, Jaji Mkuu wa Ghana, Mhe. Gertrude Sackey Torkornoo amesema lengo la Mkutano huo ni kuwaleta pamoja Majaji wa Ukanda wa Afrika kubadilishana uzoefu kuhusu Nafasi ya Majaji Wanawake katika kupambana na mila potofu katika ulimwengu wa sasa.

Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ni moja kati ya wanachama waliohudhuria katika Mkutano huo.

Mada mbalimbali zitatolewa katika Mkutano huo nazo ni pamoja na Ukatili wa mtandao; je Watoto wetu wapo salama?, umaskini na upatikanaji wa haki, kuondosha dhana hasi dhidi ya wanawake-wajibu wa Majaji, ushiriki wa  wanawake katika utawala wa Taasisi za Manispaa na kitaifa na nyingine.

 

Comments (0)

Leave a Comment