Post Details

JAJI MKUU AWAPA MADINI MAHAKAMA SACCOS

Published By:innocent.kansha

Na Innocent Kansha-Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 13 Mei, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Bodi ya Mahakama Saccos Ltd na kuahidi kuendea kuwapa ushirikiano ili ushirika huo uweze kukua na kutimiza adhima ya kuwa chama cha ushirika wa akiba na mikopo cha kuigwa na cha kisasa.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika Ofisini kwake jijini Dar es Salaam Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma amesema eneo la wanachama ambao ni watumishi wa Mahakama ni muhimu sana kwani Mahakama ina watumishi zaidi ya 5,000 lakini wanachama wa Saccos wapo 524, hii inaonyesha bado kuna mtaji mkubwa upo nje unaweza kusaidia kuongeza mtaji ushirika.

Jaji Mkuu akatoa rai kwa viongozi hao kutumia fursa za uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama hasa majengo yanayo endelea kujengwa nchi zima kubuni miradi ya kuwekeza katika maeneo hayo ili kukuza mtaji wa Saccos kama vile kuomba zabuni za ndani za kutoa huduma kwa wanachama wao.

“Nimepokea taarifa yenu imesheheni mambo mengi muhimu ya kufanyia kazi, pengine niseme tu haitokuwa sahihi kwa baadhi ya mambo kuyatolea majibu ya papo kwa papo ni vema nikae na viongozi wenzangu tujadiliane namna bora ya kutatua sehemu ya changamoto mlizowasilisha,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma amesema Mahakama itaendelea kutoa fursa mbalimbali za kuitangaza Saccos kwa watumishi na Taasisi zingine kupitia mikutano kama vile Baraza la wafanyakazi, ziara za viongozi katika maeneo mbalimbali nchini  Makongamano, Maadhimisho, Sherehe, Mikutano na maonyesho mbalimbali yanayoandaliwa na  Mahakama ya Tanzania  ili viongozi wa Saccos wapate muda wa kuhamasisha wanachama wajiunge na ushirika ili ukue.

“Nimependa sana Mwenyekiti wa Bodi alivyotoa mifano ya JMAT na TAWJA walivyoweza kusaidiwa kuimarisha umoja wao nanyi mnaomba kusaiwa kuimarisha mtaji wanu tena mnaomba kusaidiwa kwa wamu moja tu. Ninaamini hilo pia linawezekana tukishirikiana,” amesema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu amesema ana amini sana katika nguvu ya Saccos na ni njia bora inayoweza kuinua wanyonge. Ukipitia ripoti nyingi za utafiti wa REPOA sehemu ya changamoto za watumishi zimeainishwa nyingi sana, ni vema kupitia Saccos ikaleta chachu ya kutatua hizo changamoto.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama Saccos Mhe. Ferdinand Philip akisoma taarifa ya Saccos hiyo amebainisha malengo na matarajio ya uongozi wa Bodi hiyo ni kuimarisha Chama ili kukua zaidi kwa kupata wanachama wengi zaidi kutokana na mikakati iliyopo ya kutoa elimu, hamasa na uelewa zaidi juu ya manufaa mengi yatokanayo na kuwa mwanachama wa Mahakama Saccos Ltd.

“Dhima ya ushirika ni kuinua, kustawisha na kuboresha hali ya kiuchumi na kijamii kwa wanachama, kwa kuwahamasisha kuweka akiba na kuwapatia mikopo yenye manufaa na riba nafuu pamoja na huduma zingine za kifedha kwa kutumia mfumo wa teknolojia ya kisasa,” amesisitiza Mhe. Philip.

Mhe. Philip amesema maendeleo ya Chama ni makubwa kwani Chama kimeendelea kuboresha huduma za mikopo ili kuwawezesha wanachama wake kiuchumi. Aidha, katika kipindi cha kuanzia Januari, mwaka 2024, chama kimeweza kukusanya kiasi kikubwa cha fedha kama ilivyoainishwa na takwimu fedha kama ifuatavyo; Akiba ya wanachama ni shilingi 1,166,321,000/-, Hisa za Wanachama ni shilingi 30,750,000/-, Wadai na malipo ya mbele ni shilingi 98,472,160/- na Riba tarajiwa isiyoiva ni shilingi 102,904,692/-.

Kwa upande wa manufaa wanayopata wanachama wa Mahakama Saccos Ltd, Mhe. Philip amesema kuwa, wanachama wa Mahakama Saccos Ltd ambao ni watumishi wa Mahakama ya Tanzania, wameweza kupata mikopo mbalimbali yenye riba na masharti nafuu, ambayo imeweza kutatua mahitaji yao ya kifedha na kuweza kufanikisha mambo mbalimbali kama vile: kuanzisha miradi mbalimbali ya kibiashara, kununua viwanja vya makazi na kujenga nyumba zao za kuishi

Mafanikio mengine ni kama kujiendeleza kielimu, kuwasomesha watoto na wategemezi wao, kununua vyombo vya usafiri, kuwawezesha watumishi wapya kupata fedha za kuanzia maisha na kupata mikopo ya dharula kwa ajili ya matibabu ya ndugu na familia zao, ameongeza Mwenyekiti wa Bodi.

Mhe. Philip amesema, eneo lingine la faida kwa wanachama ni elimu na mafunzo ya ushirika, biashara na ujasiriamali yanayopatikana kwa kuwa mwanachama wa Mahakama Saccos Ltd. Elimu na mafunzo hayo ni kama, matumizi bora ya mikopo wanayokopa, uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya kibiashara yenye tija. Usimamizi bora wa miradi wanayoianzisha, udhibiti wa mitaji, elimu ya ujasiriamali na elimu ya maisha baada ya kustaafu.

Comments (0)

Leave a Comment