Post Details

MAJAJI, MAHAKIMU WANAWAKE TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO WA ‘IAWJ’ ACCRA GHANA

Published By:Mary C. Gwera

Na Mary Gwera, Mahakama-Accra-Ghana

Majaji na Mahakimu Wanawake wa Mahakama ya Tanzania wanatarajia kuungana na Majaji wanawake wenzao kutoka Ukanda wa Afrika kushiriki katika Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani (IAWJ) utakaofanyika jijini Accra nchini Ghana.

Akizungumza katika mahojiano maalum leo tarehe 12 Mei, 2024, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel amesema kuwa, Mkutano huo unatarajiwa kuanza rasmi kesho tarehe 13 hadi 18, Mei, 2024 na utafunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. Nana Addo Dankwa Akufo-Addo.

“Mkutano huu ni wa Kikanda kwa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake, Mkutano huu unakutanisha wanachama Majaji na Mahakimu wanawake Afrika kwa ujumla. Kwa upande wa Tanzania tutakaoshiriki katika Mkutano huo ni 18 na idadi hii imejumuisha na wenzetu wa Zanzibar,” amesema Mhe. Sehel.

Mwenyekiti huyo ameeleza kwamba, katika Mkutano huo, Mahakama ya Tanzania itapata nafasi ya kutoa mada ya kuelezea hatua zinazochukuliwa na TAWJA katika kumpa nafasi mwanamke kwenye Uongozi hasa kwenye Mahakama.

Kaulimbiu ya Mkutano huo inasema ‘Nafasi ya Majaji Wanawake katika kupambana na mila potofu katika ulimwengu wa sasa.’

Mbali na TAWJA, Vyama vingine vitakavyoshiriki katika mkutano huo ni kutoka Nigeria, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Cote d’Ivoire na nyingine.

Kiongozi wa msafara wa wanachama wa TAWJA, Mhe. Sehel pamoja na wenzake wamewasili leo hii jijini Accra majira ya saa 5 asubuhi tayari kwa kushiriki kikamilifu Mkutano huo muhimu.

 

Comments (0)

Leave a Comment