Published By: | Mary C. Gwera |
---|
Na Naomi Kitonka, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Ndoa na Familia- Temeke
Wasajili wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Masuala Ya Ndoa na Familia- Temeke pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama ya Mwanzo na ya Wilaya wanaohudumu katika Kituo hicho wameagizwa kuhakikisha uandaaji wa taarifa zote za majalada ya Ndoa na Mirathi kila mwezi unafanyika kwa usahihi na kwa wakati ili kuwa na takwimu sahihi za mashauri hayo.
Agizo hilo limetolewa tarehe 15 Aprili, 2024 na Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala Ya Ndoa na Familia- Temeke wakati wa kikao cha kujadili maendeleo ya Kituo hicho katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka kuanzia Januari hadi Machi, 2024 kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano uliopo ndani ya Kituo hicho.
Kadhalika, Mhe. Mnyukwa alimtaka Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. John Msafiri kusimamia utaratibu mzuri kwa wateja ili kupunguza msongamano katika Mahakama ya Wilaya wanaposubiri kujibiwa pale wanapofungua mashauri kwenye Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) sambamba na kutoa elimu kwa wateja na Mawakili juu ya Mfumo huo ili kuwasaidia kufungua mashauri popote walipo.
“Ni vizuri kwa Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Wilaya kusimamia vizuri utaratibu wa kuwaongoza wateja pale wanapofungua mashauri katika Mfumo wetu wa ‘e-CMS’ na kupunguza msongamano wa wateja katika makorido kwa sababu lengo la Mfumo ni kuwasaidia kufungua mashauri popote walipo na kufuatilia taratibu zote pasipo kufika mahakamani,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.
Aliongeza kuwa, hatua hiyo itawasaidia Wasajili kujibu na kupanga mashauri pasipo msukumo ‘pressure’ kutoka kwa wateja au Mawakili.
Aidha, katika kikao hicho kilitumika kama sehemu ya kupima ufanisi wa Kituo sambamba na kuweka maazimio ili kuhakikisha wateja wanafutwa machozi kama kauli mbiu ya Kituo hicho inavyosema, kutoa haki kwa wananchi kwa muda unaotakiwa na kuongeza ufanisi wa Kituo katika ngazi zote za utendaji.
Kikao hicho kiliendeshwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Jaji Mfawidhi, Mhe. Mnyukwa ambapo alipokea taarifa mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za kimahakama na kiutawala kutoka Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama Kuu na Mahakama ya Watoto na wajumbe ambao pia walipata nafasi ya kuchangia na kupokea maelekezo ya Kikao.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Kaimu Mtendaji wa Kituo, Bi. Ntuli Mwakipesile, Naibu Wasajili, Naibu Wasajili wa Kituo hicho, Mhe. Frank Moshi na Mhe. Evodia Kyaruzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya, Mhe. John Msafiri, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Aloyce Mwageni akiambatana na Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Watoto, Mhe. Vicky Mwaikambo, Maafisa Utumishi na Utawala kutoka Mahakama Kuu na Mahakama ya Watoto pamoja na Wakuu wa Vitengo na Wawakilishi wa Vyama vya Wafanyakazi katika Kituo hicho.
(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)