Post Details

BARAZA LA WAFANYAKAZI LINALENGA KUKUZA UWAZI, UWAJIBIKAJI; JAJI NANGELA

Published By:innocent.kansha

Na Fredrick Mahava-Mahakama, Sumbawanga

Baraza la wafanyakazi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga lilikutana jana tarehe 15 Aprili 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama kuu, Kanda ya Sumbawanga kujadili masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Akizungumza wakati wa kufungua Baraza hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe.Dkt. Deo Nangela alisema utaratibu wa kuwa na mabaraza unalenga kukuza uwazi na ushirikishwaji katika maamuzi mbalimbali ya utendaji kazi wa kila siku.

Mhe. Dkt. Nangela alihimiza menejimenti ya Mahakama Kanda ya Sumbawanga na Chama cha wafanyakazi (TUGHE) kushirikiana   kwa pamoja katika kutatua kero mbalimbali za watumishi ili kuongeza morali ya watumishi hao ambao ni wachache na wanafanya kazi nyingi.

“Niwakumbushe watumishi wenzangu kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kujiepusha na vitendo vya rushwa, pia mjikite katika shughuli mbalimbali za kujiongeza kipato kwani mikoa hii ya Rukwa na Katavi ina fursa nyingi,” alishauri Mhe. Dkt. Nangela

Aidha, wakati wa mkutano wa Baraza hilo kuliwasilishwa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama Kanda ya Sumbawanga kwa kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi, 2024 ambayo iliwasilishwa na Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Bi. Irene Mlangwa

Vilevile, Wajumbe wa Baraza hilo walijadili masuala mbalimbali ikiwemo mapitio ya Bajeti, ukomo wa bajeti, utekelezaji wa bajeti, changamoto za utekelezaji wa bajeti, kupokea na kujadili hoja za watumishi na pia majibu na ufafanuzi ulitolewa na viongozi mbalimbali.

Wajumbe waliohudhuria Baraza hilo kwa pamoja walikubaliana na kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza hoja mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na pia kuboresha baadhi ya mambo wakati wa Baraza lijalo.

Comments (0)

Leave a Comment