Post Details

KLINIKI ZA SHERIA KUKUZA UPATIKANAJI HAKI – JAJI MKUU

Published By:Mary C. Gwera

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Rai imetolewa kwa Vyuo Vikuu nchini vinavyotoa Elimu ya Sheria kupitia Shule Kuu za Sheria katika Vyuo hivyo kuimarisha Kliniki za Sheria ili kukuza na kupanua wigo wa upatikanaji wa haki kwa Watanzania.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 15 Aprili, 2024 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Shule Kuu ya Sheria iliyofanyika katika ukumbi wa ‘CIVE Auditorium’ uliopo chuoni hapo.

“Mwananchi akifahamu mipaka ya sheria itamsaidia sana, msaada wa sheria ni huduma yenye umuhimu mkubwa sana, hivyo tutoe elimu pana ya kumuwezesha mwananchi wa kawaida kupata haki zake hata katika Ofisi za Umma,” amesema Jaji Mkuu.

Amesema, uwepo wa huduma za msaada wa kisheria kutoka kwa wadau mbalimbali kama Kliniki ya Msaada wa Kisheria unatoa fursa kwa wanachi wa kipato cha chini ambao wameshindwa kumudu gharama za kumuajiri Wakili, kupata haki zao na hivyo kuongeza utulivu na amani katika jamii na Nchi kwa ujumla.

Mhe. Prof. Juma amesema kwamba, Kliniki za Sheria zina faida kubwa kwa wanafunzi wanaotoa huduma kwakuwa zinawapa nafasi ya kujifunza kusaili ili wapate undani wa tatizo; inawajengea uwezo wa kuchambua na kuacha yasiyo na maana; wanaona namna Taasisi za Kisheria zinavyofanya kazi; zinawawezesha kuwaelewa wananchi wanavyotafsiri dhana na maana ya wanavyoelewa haki, inawasaidia kujenga mahusiano ya kitaaluma ambayo itawasaidia baadaye watakapojiunga na soko la ajira.

Amesisitiza kuhusu umuhimu wa elimu ya sheria kwa umma katika maeneo yenye shida hapa nchini ambayo ni pamoja na Elimu ya uraia (civic education), Ukatiba (Constitutionalism), Uwajibikaji (accountability), Unyanyasaji/Ukatili wa kijinsia (gender-based violence).

Maeneo mengine ni Haki za mtoto na binadamu kwa ujumla, Haki ardhi, Migogoro ya ardhi, Haki na ulinzi wa mlaji, Mirathi, kuepuka matumizi mabaya ya mapingamizi mahakamani na matumizi ya sababu za kiufundi kuchelewesha haki, umuhimu wa kutumia njia za Usuluhishi kutatua migogoro nje ya Mahakama, kusimamia Maadili ya Mawakili na Watumishi wa Umma na mengine.

Aidha, Mhe. Prof. Juma amewakumbusha Wanafunzi wa Taaluma ya Sheria, kuwa, Karne hii ya 21 ina mabadiliko makubwa na ushindani wa kupindukia, hivyo Elimu ya Sheria (Legal Education), Taaluma ya Sheria (Legal Profession), Upatikanaji Haki mahakamani (Access to Justice in courts) na hata Kliniki za Sheria ni lazima pia zibadilike ili ziende sambamba na ushindani wa karne hiyo.

“Ndio maana, nimewaomba waandaaji wa Siku hii ya Sheria, wamruhusu Mkuu wa Idara ya TEHAMA ya Mahakama ya Tanzania, atoe wasilisho fupi, kuhusu Matumizi makubwa ya Teknolojia, ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence) katika utoaji haki katika Karne ya 21,” amesema Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lugano Kusiluka amemshukuru Jaji Mkuu kwa kushiriki katika Siku hiyo huku akisema kuwa, Shule Kuu ya Sheria ilianzishwa mwaka 2009 kama Idara ikiwa na programu moja ya shahada ya awali ya Sheria.

“Leo ikiwa ni takribani miaka kumi na tano tangu kuanzishwa kwake, Shule hii inatoa shahada ya awali ya sheria, shahada ya umahiri katika sheria za mashirika (Masters of Laws in Coorporate Law), Shahada  ya umahiri katika sheria za haki ya binadamu (Masters of Laws in Human Rights law) na shahada ya uzamivu katika sheria,” ameeleza Prof. Kusiluka.

Aidha, Mkuu huyo wa Chuo amefikisha ombi kwa Jaji Mkuu juu ya Shule ya Sheria Tanzania (LST) kuanzisha matawi nchi nzima ili kuwawezesha wanafunzi wasio na uwezo kusoma wakiwa katika maeneo/Mikoa yao.

Kadhalika, Mkuu huyo wa Chuo ameomba pia kupatikana kwa ukumbi mkubwa zaidi wa studio ya kuendesha Mahakama kwa vitendo.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Kalege Enock ametoa mada kuhusu Safari ya Mahakama ya Tanzania kuelekea Mahakama inayotoa huduma kwa njia za Kidijitali (Judiciary of Tanzania Digital Transformation Journey). 

Katika wasilisho lake, Bw. Kalege amebainisha kuwa, Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kwenye matumizi ya TEHAMA kutokana na mambo makuu matatu (3) nayo ni pamoja na Uongozi imara na thabiti ambao umetoa ushirikiano katika eneo hilo, Mpango Mkakati wa Mahakama na Utoaji huduma kwa wananchi.

Maadhimisho hayo ni ya tatu (3) tangu kuanzishwa kwa Siku ya Sheria katika Chuo hicho. Siku ya Sheria ya Chuo hicho kwa mwaka huu imebebwa na Kaulimbiu isemayo; Uimarishaji wa Kliniki za Sheria Vyuo Vikuu katika kukuza na kupanua wigo wa upatikanaji haki Tanzania.

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment