Post Details

VIONGOZI WA MAHAKAMA KANDA YA KIGOMA WAKUTANA

Published By:Mary C. Gwera

  • Waweka mikakati ya kutoa haki kwa wakati
  • Matumizi ya TEHAMA yaendelea kusisitizwa

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, hivi karibuni ameongoza kikao cha Viongozi wa Kanda hiyo kilicholenga kujadili utekelezaji wa shughuli za Mahakama na kuweka mipango ya pamoja ya utekelezaji wake.

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Mahakama ya Wilaya Kakonko ambapo Jaji Rwizile aliwakumbusha wajumbe wa kikao hicho kutumia pia Mifumo ya TEHAMA kwa asilimia 100 ili kuleta matokeo chanya ya utekelezaji wa dira ya mahakama ya utoaji wa haki kwa wakati.

“Miundombinu ya TEHAMA na vifaa vyake viwe ni kipaumbele namba moja katika bajeti zetu maana ndio nyenzo kubwa ya utoaji wa huduma kwa wananchi, tukumbuke kuwa Mahakama ya Tanzania imejikita kutoa huduma za Mahakama kwa njia ya Mifumo mbalimbali ambayo imeshuka mpaka Mahakama za mwanzo, hivyo uimara wa huduma zetu unategemea uwepo na ubora wa miundombinu na vifaa vyake,” alisema Jaji Rwizile.

Aliongeza kuwa, Mahakama Kanda ya Kigoma inapaswa kujihakikishia inakuwa na vifaa wezeshi na bora vinavyoendana na kasi ya maboresho ya Mahakama Mtandao huku akiwasihi wajumbe wa kikao kuweka kipaumbele manunuzi ya Jenereta(standby Generator) na kompyuta mpakato (laptop) za akiba ikiwa ni mbadala pale ambapo umeme unakuwa haupo katika vituo hivyo, ili kuweka uhakika wa kuendelea kuwahudumia wananchi kupitia Mfumo wa Ki-elektroniki wa Usimamizi wa Mashauri ( e-CMS).

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho, Mhe. Rwizile aliwasisitiza Viongozi hao kusimamia ushirikiano na nidhamu kwa watumishi walioko chini yao na kuongeza mawasiliano ili kusaidia kutatua kwa haraka changamoto wanazokutana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kadhalika aliwataka pia kuwa wabunifu na kubuni njia mbadala za kupokea na kutatua malalamiko kutoka kwa wanannchi na wadau ikiwa ni pamoja na kutunza takwimu ili kuendelea kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama nguzo namba tatu.  

Akizungumzia kuhusu rasilimali fedha inayopatikana, alisema ielekezwe katika vipaumbele kwanza ambavyo vitahakikishia uhakika wa shughuli za kusikiliza mashauri yaliyopo katika Vituo katika Wilaya zote.

Aidha, aliwataka Mahakimu wa Wilaya zote katika Kanda hiyo kuwakumbusha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo zote kusimamia ufungwaji wa mashauri ya Mirathi na kuhakikisha wadaawa wamelipwa mirathi zao ili kuondoa uwepo wa mashauri hayo kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki, alisisitiza kuhusu matumizi ya Mfumo wa Ki-elektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) ili kuhakikisha kila Kituo kimesajili na kusikiliza mashauri yote mtandaoni.

Wajumbe waliohudhuria katika kikao hicho kwa pamoja walikubaliana na kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza ili kuifanya Kanda ya Kigoma kuwa ya mfano katika utendaji kazi na kumhudumia mwananchi ili hatimaye lengo la utoaji wa Haki kwa wakati liweze kufikiwa.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kanda ya Kigoma akiwemo Naibu Msajili, Mhe Gadiel Mariki, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe Rose Kangwa, Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu, Uvinza, Buhigwe, Kigoma pamoja na Wakuu wa Vitengo.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Comments (0)

Leave a Comment