Post Details

JAJI MAGHIMBI AFANYA UKAGUZI GEREZA LA MIFUGO UBENA BWAWANI

Published By:Mary C. Gwera

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amefanya ukaguzi katika Gereza la Mahabusu la Mifugo Ubena lililoko maeneo ya Bwawani Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Akizungumza na Mahabusu pamoja na Wadau wa Haki Jinai katika Gereza hilo jana tarehe 28 Machi, 2024, Mhe. Maghimbi alisema, lengo la ukaguzi huo ni kupata matatizo ya jumla au changamoto ambazo zinawakabili Mahabusu na Wafungwa ambao wamekata rufaa.

Awali akimkaribisha Jaji Mfawidhi ofisini kwake, Mkuu wa Gereza hilo Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Godwin Mekoki alisema Gereza hilo lenye hekari 10,600 lilianzishwa mwaka 1964 kwa madhumuni ya kuhifadhi wafungwa watumishi wa Serikali ila kwa sasa linahifadhi wafungwa pamoja na Mahabusu wenye mashauri mbalimbali.

Akisoma taarifa yake mbele ya Jaji Mfawidhi, Mrakibu Mekoki alisema  hali ya usalama wa Gereza kwa ujumla ni salama, Maafisa na Askari wanashirikiana vizuri kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama wa mali za Serikali unaimarika.

Aidha, alieleza pia changamoto zinazolikabili Gereza hilo kuwa ni pamoja na usafiri wa kupelekea mahabusu mahakamani ambapo kwa sasa wanatumia gari aina ya Isuzu Fuso na Toyota Land Cruiser ambayo sio rafiki kiusalama kwa kusafirishia Mahabusu kwa kuwa lipo wazi.

“Changamoto nyingine ni mafuta (Diesel) kwa ajili ya magari yanayopelekea  Mahabusu bado hayatoshelezi  hii ni kutokana na umbali wa Mahakama pamoja na kuwa na safari nyingi,” alieleza Mkuu huyo wa Gereza.

Baada ya kusikiliza taarifa hiyo, Mhe. Maghimbi alitatua baadhi ya changamoto zilizoonekana ziko ndani ya uwezo wake kwa wakati huo na zile zilizokuwa zinahitaji kushughulikiwa zaidi aliahidi kuwapa majibu mapema iwezekanavyo.

Kadhalika alitoa anuani ya barua pepe ili kama changamoto ikitokea ikashindwa kushughulikiwa kwa ngazi ya Wilaya na Mkoa basi apewe taarifa kwa njia ya barua pepe na atashughulikia kwa wakati na sio kusubiri tu ukaguzi ndio changamoto zitolewe.

Jaji Mfawidhi huyo aliwajulisha pia Maafisa wa Magereza wanaoshughulikia Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) kuhudhuria Semina itakayoandaliwa kwa ajili ya Maafisa wa Magereza wanaoshughulikia rufaa za wafungwa.

Akijibu lalamiko la Mahabusu aliyelalamikia kutoelewa Lugha iliyoandikwa katika hukumu, Mhe. Maghimbi alisema baadhi ya Mahakama zimeanza kufunga Mifumo ya Kutafsiri, hivyo kuweka uelewa wa kile kilichoandikwa katika hukumu lakini pia aliwaomba Askari Magereza kuwasaidia kutafsiri.

 Katika ziara yake, Jaji Maghimbi aliongozana na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Sundi Fimbo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Sameera Suleimani, Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Pwani, Bw. Moses Minga pamoja na Wadau wa Haki Jinai wa Mkoa wa Pwani.

Comments (0)

Leave a Comment