Post Details

MKAKATI KUUNGANISHA MFUMO WA MAKTABA MTANDAO, TANZLII UPO MBIONI

Published By:Mary C. Gwera

Na Tawani Salum-Mahakama

Mahakama ya Tanzania na Viongozi wa Mfumo wa Sheria na Maamuzi Africa (AfricanLII) wapo katika mkakati wa kuunganisha Mfumo wa Maktaba Mtandao na Mfumo wa Mahakama unaochapisha maamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni (TanzLII) ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kisheria na kufanyika kwa tafiti.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Maktaba Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam jana tarehe 27 Machi, 2024, Mkurugenzi wa AfricanLII, Bi. Mariya Badeva alisema kuwa uunganishwaji wa mifumo hiyo utasaidia upatikanaji wa taarifa za kisheria kwa wakati na kurahisisha zoezi zima la ufanywaji wa tafiti kuwa wa haraka na uhakika.

 ‘’Uunganishaji wa mifumo hii utapunguza kazi kubwa zinazofanywa na Makatibu wa Majaji na Wakutubi katika kupandisha maamuzi kwenye mifumo na badala yake taarifa za kisheria zitahama moja kwa moja kutoka katika Maktaba Mtandao kwenda kwenye mfumo wa TanzLII kwa haraka na wakati,’’ alisema.

Bi. Mariya aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kusaidiana nao kwa kila hatua ili kufanikisha mpango mkakati huo. Alitanabaisha kuwa ndani miezi mitatu mifumo hiyo itasomana na kusababisha utendaji ndani ya Mahakama kuwa wa kasi na wenye tija kwa jamii kwa ujumla.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kifungu Kariho alieleza kuwa uunganishaji wa mifumo hiyo utasaidia kuharakisha ufanyaji wa tafiti za kisheria na kuwezesha upatikanaji wa haki kwa haraka.

Alibainisha kuwa zoezi hilo lipo katika aina mbili, ikiwemo uunganishaji wa Mfumo wa kusimamia na kuendesha mashauri na Maktaba mtandao na awamu ya pili ya kuunganisha Maktaba Mtandano pamoja na TanzLII.

Mhe. Kariho alisema kuwa kukamilika kwa uunganishaji wa mifumo hiyo utaleta tija kwa Mahakama yenyewe na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kiongozi wa timu ya uundaji wa mifumo wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Samweli Mshote alisema kuwa matayarisho yote yapo tayari kwa ajili ya zoezi hilo.

Alisema kuwa kinachosubiliwa ni ruhusa kutoka katika Mamlaka ya Serikali Mtandao (EGA) yenye mamlaka ya kuratibu na kusimamia mifumo yote ya kiserikali Tanzania.

Comments (0)

Leave a Comment