Post Details

MAHAKAMA MANYARA YAFANYA UKAGUZI WA MAHAKAMA NA MAGEREZA

Published By:innocent.kansha

Na Christopher   Msagati- Mahakama, Manyara

Mahakama Kuu Manyara imefanya Ukaguzi katika Robo ya kwanza ya Mwaka 2024 kuanzia tarehe 25 Machi, 2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Mbulu, Hanang, Mahakama za Mwanzo pamoja na Magereza ya Wafungwa na Mahabusu katika Wilaya hizo.

Azungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ukaguzi huo Mahakama ya Wilaya ya Mbulu, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora aliwapongeza watumishi wa Wilaya hiyo kwa utendaji kazi mzuri unaochangia mafanikio ya Kanda nzima hususani kwa kumaliza mashauri kwa wakati na kupunguza malalamiko ya wadaawa wanaofika Mahakama kila siku.

“Kwa kweli kazi mnayofanya ni kubwa na mafanikio yanaonekana, kwa kipindi hiki tunaona kuwa mashauri yanaenda kwa kasi na jambo hili limepunguza hata idadi ya Mahabusu katika gereza. Hili linaenda sambamba na upunguaji wa malalamiko katika Ofisi zetu,” aliongeza Mhe. Kamuzora.

Zoezi hilo pia, lilifanyika katika Mahakama ya Mwanzo Endagkot na Gereza la Wilaya ya Mbulu. Akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi wa gereza la Wilaya ya Mbulu, Kaimu Mkuu wa Gereza la Mbulu Bw. Erick Pallangyo alipongeza uamuzi wa Mahakama wa kufika Gerezani hapo na kusikiliza matatizo ya mahabusu na wafungwa ambao wachache wao wanasubiri kupatiwa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri yao ili wawaeze kukata rufaa za mashauri yanayowakabili kwa wakati. Mahakama kupitia ujumbe huo uliahidi kulifanyia kazi jambo hilo ndani ya muda mfupi kupitia Uongozi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu.

“Mheshimiwa Jaji ujio wako umeturahisishia kupata majibu ya maswali ambayo yalikuwa yanaulizwa mara kwa mara na wafungwa na maabusu wa gereza hili ni matumaini yetu kuwa kila mtu ameridhika kutokana na majibu na maelezo ambayo mmeyatoa”, alisema Bw. Pallangyo.

Akiwa katika ukaguzi wa Mahakama ya Wilaya ya Hanang na Mahakama ya Mwanzo Katesh, Mhe. Kamuzora alikutana na changamoto ya mahabusu kutokupelekwa Mahakamani kwa wakati, ikiwa ni kwa sababu Wilaya ya Hanang haina Gereza la Wilaya hivyo kulazimika mahabusu kuhifadhiwa katika Gereza lililopo wilayani Babati. Akitolea ufafanuzi hoja hiyo, Mhe. Kamuzora aliiahidi kulifikisha suala hilo kwa Viongozi husika ili kuona namna bora ya kutatua changamoto hiyo.

Mhe. Kamuzora alisisitiza mpangilio bora wa masijala, usafi wa mazingira ya Ofisi, kuongeza uwajibikaji na ushirikiano katika utendaji kazi wa kila siku kwa ajili ya kusaidia kufikisha malengo ya Mahakama.

Aidha, ziara hiyo ya Ukaguzi pia ulihusiha ukaguzi wa maendeleo ya miradi ya ujenzi ambayo imeanza hivi karibuni katika Mahakama za Wilaya ya Mbulu na Hanang na kuwasisitiza Wakandarasi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kukamilisha ujenzi huo ili majengo hayo yanze kutumika.

Wakati leo tarehe 27 Machi, 2024 zoezi la ukaguzi limeendelea katika Gereza la Babati mjini kwa ajili pia ya kusikiliza kero na maoni mbalimbali kutoka kwa wafungwa na mahabusu wa Gereza hilo na kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali yaliyohojiwa.

Ukaguzi huo umeongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Manyara, Mhe. Bernard Mpepo, Msaidizi wa Sheria Mhe. Thobias Kavishe, Mtendaji wa Mahakama Kuu Manyara, Bw. Jacob Swalle na Afisa Tawala Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Bw. Christopher Msagati.

Comments (0)

Leave a Comment