Post Details

AFRICANLII, MAHAKAMA YA TANZANIA KUJADILIANA UCHAMBUZI DATA KUPITIA MFUMO WA TANZLII

Published By:Mary C. Gwera

Na Salum Tawani-Mahakama, Maktaba

Mahakama ya Tanzania ipo katika majadiliano na Viongozi wa Mfumo wa Sheria na Maamuzi Afrika (AfricaLii) kuhusu uchambuzi wa data katika Mfumo wa Mahakama unaochapisha maamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni (TanzLII) ili kuboresha upatikanaji wa taarifa zitakazorahishia utendaji wa kazi.

Akizungumza katika majadiliano yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya New Africa Four Points jijini Dar es Salaam jana tarehe 26 Machi, 2024, Mkurugenzi wa AfricanLII, Bi. Mariya Badeva alisema kuwa uchambuzi wa data kupitia Mfumo wa TanzLII (Data Analytic) utasaidia kuongeza kasi katika utaoaji wa haki ndani ya Mahakama ya Tanzania,

“Kupitia Mfumo huu watendaji wa juu wa Mahakama watakuwa kwenye wakati mzuri kujua ni eneo gani hawakufanya vyema na eneo lipi wamefanya vizuri, hivyo kusaidia katika kuboresha huduma za kimahakama na jamii kwa ujumla,” alisema.

Bi. Mariya alimpongeza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza kwani ndiye aliyehusika katika kuanzisha Mfumo huo, huku Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Kifungu Kariho na Bw. Salum Tawani wakihakikisha unasimama na kuwasaidia Majaji na wadau wengine kwenye fani ya sheria kufanya tafiti kwa wakati.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Kihwelo, akizungumza wakati wa ukaribisho alisema kuwa uchambuzi wa data kupitia Mfumo wa TanzLII, unawaweka Watendaji wa Mahakama katika wakati muafaka na kufikiri kwa kina namna makosa yanavyofanyika na sababu makosa ya kiufundi yanavyosababisha shauri kuondoshwa badala ya kuangalia namna bora shauri la msingi linavyotatuliwa.

Jaji Kihwelo alionesha kutopendelea makosa ya kiufundi kutumika kuondosha mashauri na na badala yake itumike njia ya kawaida ya kusikiliza shauri la msingi na hatimaye kufikia uamuzi (substantive objective).

Naye Mhe. Kahyoza, akizungumza wakati wa majadiliano hayo, alisema kuwa uchambuzi wa data kupitia Mfumo wa TanzLII unawapa taarifa Watendaji namna gani Mahakama ya Tanzania inafanya kazi.

“Mfano, kwenye eneo la mashauri ya ubakaji, kwanini waliotenda vitendo hivyo wanaachiwa huru au kwanini baadhi ya kanda kunakithiri vitendo vya ubakaji. Uchambuzi wa data kwenye mfumo wa TanzLII utaonyesha Kanda ambazo kuna mashauri mengi ya ubakaji, hivyo Watendaji kuwa katika wakati mzuri kuangalia namna ya kuzimaliza changamoto hizi,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kifungu Kariho alisema kuwa uchambuzi wa data kupitia Mfumo wa TanzLII utasaidia kujua madhaifu na mafanikio katika utendaji wa kazi ndani ya Mahakama.

Alisema kwamba hatua hiyo itawezesha changamoto zinazojitokeza kubainishwa na kuiwezesha Mahakama kuwa katika nafasi nzuri ya kuzifanyia kazi na kuleta tija ndani ya Mahakama na jamii kwa ujumla.

Mhe. Kariho alibainisha kuwa uchambuzi wa data kupitia Mfumo wa TanzlII usiishie kwenye mashauri ya jinai pekee, bali pia kuangalia katika mashauri ya madai.

Wakili kutoka Ubalozi wa Uingereza, Bw. Andrew Stephens alisema kuwa uchambuzi wa data kutoka katika Mfumo wa TanzLII utaimarisha utendaji na kuwezesha kujua kwa namna gani waliokata rufani walishinda na kutolewa gerezani.

Alieleza kuwa kupitia uchambuzi huo Mahakama itaweza kujua muda ambao shauri linachukua tangu kufunguliwa hadi kumalizika huku mfumo ukionyesha kila kitu kinachofanyika.

Hatua hii inawasaidia watendaji wa juu ndani ya Mahakama kuangalia namna bora ya kufupisha muda wa usikilizwaji wa shauri kama itaonekana inachukua muda mrefu kabla ya kumalizika.

Comments (0)

Leave a Comment