Post Details

MFUMO WA TAFSIRI, UNUKUZI ZANA MUHIMU KATIKA MCHAKATO WA HAKI

Published By:innocent.kansha

Na. FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Asina Omari amehimiza mfumo wa tafsiri na unukuzi kutumika kikamilifu kwani ni zana muhimu katika kufanikisha mchakato wa haki mahakamani.

Mhe. Asina ametoa wito huo leo tarehe 1 Machi, 2024 alipokuwa anafungua mafunzo ya siku mbili ya usimamizi na matumizi ya mfumo wa tafsiri na unukuzi mahakamani yanayofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

“Tunafahamu kuwa tafsiri na unukuzi ni zana muhimu katika kufanikisha mchakato wa haki mahakamani. Kwa hivyo, ni jukumu letu kama watoa huduma za Mahakama kuhakikisha mfumo huu wa tafsiri na unukuzi unatumika ipasavyo kama ilivyokusudiwa,” amesema.  

Jaji Asina amebainisha kuwa mfumo huo unawezesha mawasiliano sahihi kati ya wahusika wote, kutoka kwa Majaji na Mawakili hadi kwa mashahidi na washiriki wengine katika usikilizaji wa mashauri.

“Katika mafunzo haya, tutazingatia mambo ya msingi katika tafsiri na unukuzi kupitia mfumo wa kielektroniki. Tunataka kuhakikisha kuwa tunaendelea kutoa huduma bora kwa wale wote wanaohitaji upatikanaji wa haki katika Mahakama zetu kote nchini,” amesema.

Hivyo, Mhe. Asina akawasihi washiriki hao wa mafunzo kuchukua fursa hiyo kujifunza na kushirikiana, kwani kwa kufanya hivyo kutaiwezesha Mahakama ya Tanzania kufikia lengo lake la kutoa haki kwa kila mtu, bila kujali lugha au utaifa.

Kadhalioka, amewaasa kutumia fursa hiyo waliyoipata kuonesha mamlaka zilizowateua kuwa hawakukosea kuwapa nafasi hiyo ya kusimamia matumizi ya mfumo huo ili kuharakisha utoaji haki kwa kila mtu na kwa wakati.

Mhe. Asina akabainisha pia kuwa mafunzo hayo yanajiri katika wakati ambapo mahitaji ya tafsiri na unukuzi katika mifumo ya kisheria yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sambamba na ukuaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani. 

“Ni muhimu kuzingatia mbinu sahihi za kuhakikisha kuwa haki za kila mtu zinaheshimiwa na kudumishwa kwa njia inayofaa na yenye heshima. Tushirikiane kufanya   Mahakama zetu kuwa sehemu ya haki na usawa kwa kila mtukupitia njia zote za teknolojia,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha, akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji Asina kufungua mafunzo hayo, alisema kuwa kazi kubwa watakayokuwa nayo washiriki hao ni kusimamia matumizi ya vifaa katika Mahakama zao na watahitajika kutoa taarifa kila baada ya muda watakaopangiwa.

“Pia watahakikisha wanawasilisha changamoto zote za matumizi ya mfumo huu. Itategemea changamoto hizo kama ni za kitehama itabidi kwanza zipitie kwa maafisa TEHAMA katika maeneo nyao na zifikishwe makao makuu kama itashindikana kupatiwa ufumbuzi,” amesema.

Mhe. Kamugisha amewahimiza pia washiriki hao watakapohitimu mafunzo hayo kuratibu matumishi ya mfumo huo kwani vifaa hivyo vimefungwa kwenye kumbi za wazi ambazo ni chache ukilinganisha katika baadhi ya Mahakama kunakuwa na Majaji na Mahakimu ambao ni zaidi ya seti za vifaa vilivyofungwa.

“Hivyo, tunategemea wao ndio watakaokuwa wanaratibu nani anaingia mahakamani ili kuwarahisishia Majaji au Mahakimu kutogongano,” amesema na kuwaomba wahitimu kwenda kuwafundisha wenzao ambao hawakupata fursa hiyo ili kuweza kupanua uwigo wa uelewa kwa watumishi wengine.

Awali, akieleza maneno ya utangulizi, Mratibu wa Mafunzo, Bw. Donbosco Gama alimweleza Jaji Asina kuwa mafunzo hayo yamewaleta kwa pamoja washiriki 23 yanayojumuisha Wasaidizi wa Sheria wa Majaji 11 na Wasaidizi wa Kumbukumbu 12 ambao wamechaguliwa kutoka katika Mikoa mbalimbali nchini baada ya kupitia kwenye mchujo mkali miongoni mwa wengi mliopo katika vituo vyao vya kazi.

Comments (0)

Leave a Comment