Post Details

JAJI MKUU AWATAKA WADAU MNYORORO WA UTOAJI HAKI KUWA WAADILIFU

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi na Seth Kazimoto- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Arusha

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wadau wote kwenye mnyororo wa utoaji haki kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao ili kutenda haki kwa wananchi.

Akifungua mafunzo ya siku mbili  ya  kuwajengea uwezo watakaokuwa Wakufunzi wa Kamati za Maadili za Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ambayo yanawalenga Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu zikiwemo Divisheni za Mahakama Kuu na Kituo cha Usuluhishi, Jaji Mkuu amesema wadau wa utoaji haki wakikosa uadilifu, Mahakama ndiyo hulaumiwa kwa kutokutenda haki.

”Kama walivyo Majaji, Wasajili, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama; Wapelelezi, Waendesha Mashtaka, Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea, Madalali wa Mahakama, na Wasambaza Nyaraka, wanatakiwa kuwa na sifa ya uadilifu, weledi, uwajibikaji, kuaminika, na kutegemewa kuwa watatenda haki” alisema Jaji Mkuu.

Aliwataka wadau katika mnyororo wa utoaji haki kusimamia kanuni zao za maadili na kuchukuliana hatua wao wenyewe wanapokiuka maadili yao. Aidha Jaji Mkuu pia aliwataka wananchi kuwa waadilifu.

”Kwa mfano Mwananchi ana kesi inayoendelea mahakamani, au anayo nafasi ya kukata rufani- lakini ataandika barua kwa Mhe. Rais, Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi kuwaomba “waingilie kati”. Maombi ya aina hii ni uvunjifu wa maadili” alisema.

 Aidha, Jaji Mkuu amewataka Wanahabari nchini kutoa kwa usahihi taarifa zinazohusu Mhimili wa Mahakama kwa kuhusisha pande zote mbili ili kutenda haki badala ya kutoa taarifa zinazoegemea upande mmoja. Alisema ni muhimu jamii ikaelimishwa kuwa wao ni sehemu ya kujenga maadili kwa Maafisa Mahakama kwa kuepuka kuwashawishi kuvunja maadili kwa kutoa uamuzi kwa upendeleo.

Akizungumzia mafunzo hayo, Jaji Mkuu alisema jitihada za Tume kutoa mafunzo hayo ni kielelezo dhahiri na dhamira ya dhati ya  kuhakikisha kuwa suala la maadili, uadilifu na uwajibikaji linaeleweka katika ngazi zote za Mahakama na Kamati za Maadili za Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ili uelewa huo ukatumike  kuendelea kulinda heshima ya Mahakama.

Alisema Majaji Wafawidhi ni kiungo muhimu kinachowakilisha uongozi wa Mahakama, na pia Tume katika usimamizi imara wa maadili ya watumishi na Maafisa-Mahakama katika Kanda.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011, Majaji Wafawidhi ndio wenye jukumu la kuwasilisha Tume ya Utumishi wa Mahakama, taarifa ya uchunguzi wa mashauri ya kinidhamu kutoka kwenye Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Mkoa au Wilaya. Aliongeza kuwa, taarifa ya Kamati inayowasilishwa Tume inatakiwa pia kuwa na taarifa ya Jaji Mfawidhi kuhusu mwenendo wa Afisa Mahakama mwenye shauri husika.

“Hivyo, mafunzo haya ya siku tatu ni muhimu kwenu sio tu kwa ajili ya kutekeleza jukumu la kuwafundisha Wajumbe wa Kamati za Maadili ngazi ya Mkoa na Wilaya bali kwa kuwa ninyi pia walezi katika masuala ya nidhamu na maadili kwa watumishi wa Mahakama na wadau wa Mahakama katika mnyororo wa utoaji haki”, alisema.

Mwenyekiti huyo wa Tume alisema Kamati za maadili ni jicho la Tume katika kusimamia, kuendeleza na kudumisha maadili ya Utumishi wa Mahakama ili kuufanya utumishi wa Mahakama kuwa wenye heshima, uadilifu, weledi, na uwajibikaji.

Prof. Juma alisema kamati za Maadili zimepewa wajibu wa kisheria, wa kuishauri Tume kuhusu uzingatiaji wa Maadili ya Utumishi wa Mahakama ili watoe huduma bora kwa jamii ya Watanzania.  

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amesema maadili ni moja kati ya nguzo muhimu za Mahakama ya Tanzania katika kuboresha huduma na kuimarisha taswira chanya ya Mhimili huo.

Aliwataka watumishi wote wa Mahakama ya Tanzania kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ili wananchi wapate huduma bora na kujenga imani na Mhimili huo wenye jukumu la msingi na la kikatiba la kutoa haki.

Mafunzo ya siku mbili kwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu kutoka maeneo mbalimbali nchini yanalenga kuwajengea uwezo Majaji hao wa kutoa mafunzo yanayofanana (equal standard) kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mkoa na Wilaya katika mikoa yote nchini.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni   kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.

Jukumu la kusimamia maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na.4 ya mwaka 2011.

 

Comments (0)

Leave a Comment