Post Details

WANANCHI MKOANI KIGOMA WASHUHUDIA HUKUMU IKISOMWA KWA NJIA YA MTANDAO

Published By:Mary C. Gwera

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Baadhi ya wananchi mkoani Kigoma wamejitokeza Mahakama Kuu ya Kanda hiyo kusikiliza usomwaji hukumu ya Bw. Moris Peter Mkazi wa Mwanga Majengo Manispaa ya Kigoma Ujiji baada ya kumkuta na hatia ya mauaji kwa kuwakata kwa kutumia kitu chenye ncha kali watu saba (7) wakazi wa Kijiji cha Kiganza Kata ya Mwandiga, Halmashauri ya Wilaya Kigoma.

Akisoma hukumu hiyo hivi karibuni, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, alisema Mahakama imetoa hukumu Shauri la mauaji namba 45 la mwaka 2022 ya kunyongwa hadi kufa kwa mshitakiwa huyo baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa mahakamani kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo kwa kukusudia na hivyo.

Aidha, wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani wananchi mbalimbali walifuatilia usomwaji wa Hukumu hiyo kwa njia ya Televisheni zilizofungwa maalum katika Mahakama hiyo ili kurahisisha usikivu na ufuatiliaji wa kikao cha Mahakama  kilichokuwa kikiendelea katika ukumbi namba moja (1) uliopo katika Mahakama hiyo.

Hata hivyo usomwaji wa hukumu hiyo ulishuhudiwa na Viongozi wa Haki Jinai, Viongozi wa Taasisi za Umma mkoani humo, Viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa jukwaa la Mawakili, vikundi mbalimbali vya burudani, klabu za wanafunzi wa Shule za Sekondari, wanahabari kutoka vyombo mbalimbali ya pamoja na wananchi kutoka sehemu maeneo mbalimbali mkoani humo.

Moja ya mwananchi ambaye hakutaka jina lake kutajwa aliipongeza Mahakama kwa kuboresha mifumo hii ya TEHAMA. 

“Nimeshuhudia jinsi ilivyosaidia mamia ya watu kuona na kusikia jinsi Jaji akisoma hukumu ya kesi ya mauaji akiwa ukumbini ghorofa ya pili na tukiwa mwanzo wa jengo (ground) zilipofungwa televisheni kwajili ya wananchi kufatilia hukumu,” alisema mwananchi huyo.

Mahakama ya Tanzania imeweka na inaendelea kuwekeza katika matumizi ya TEHAMA katika Mfumo mzima wa utoaji Haki, Mahakama imeweka mifumo ya kisasa katika kuendesha mashauri tangu kufungua shauri mpaka kutoa maamuzi (hukumu).

 

Comments (0)

Leave a Comment