Post Details

JAJI MKUU WA TANZANIA ASHIRIKI MAADHIMISHO SIKU YA SHERIA ZANZIBAR

Published By:Mary C. Gwera

 

JAJI MKUU WA TANZANIA ASHIRIKI MAADHIMISHO SIKU YA SHERIA ZANZIBAR

 

Na Mary Gwera-Mahakama, Zanzibar

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 07 Februari, 2024 ameungana na wananchi wa Zanzibar, akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kushiriki katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Visiwani humo.

Mhe. Prof. Juma pamoja na ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania alioambatana nao wameshiriki maadhimisho ya Siku hiyo katika Viwanja vya Mahkama Kuu ya Zanzibar iliyopo eneo la Tunguu Mkoa wa Kusini.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameziagiza Taasisi za Sheria Visiwani humo kuhakikisha kuwa, mchakato wa utungaji Sheria ya kuundwa kwa Mahakama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi unakamilika haraka iwezekanavyo.

“Katika salaam za Jaji Mkuu wa Zanzibar, ameeleza kuwa, agizo langu la kuundwa kwa Mahakama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi limeanza kufanyiwa kazi na kwa sasa rasimu ya Sheria hiyo imeshaandaliwa, hivyo ni naagiza mchakato huo kukamilika mapema,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.

Katika hotuba yake, Rais Mwinyi amekiri kufurahishwa na Kauli Mbiu ya Siku ya Sheria isemayo ‘Mazingira bora ya kazi, maadili, uwazi na uweledi huashiriab upatikanaji wa haki, huvutia uwekezaji na ukuaji wa uchumi.’

 

“Nimefurahishwa sana na Kauli Mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Sheria, hivyo tunapaswa kufahamu kuwa, kwa sasa nchini mwetu kumekuwa na ongezeko la wawekezaji ambao wanawekeza katika Sekta mbalimbali kama vile ujenzi wa mahotel, viwanda na kadhalika, utekelezaji wa mambo yote hayo lazima uende sambamba na mifumo mizuri ya upatikanaji wa haki itakayohakikisha kuwa, haki inapatikana kwa haraka na kwa uwazi, kwa urahisi na kwa ubora wa hali ya juu,” amesisitiza Rais Mwinyi.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali inasisitiza kuhusu matumizi ya njia mbadala ya utatuzi wa migogoro (Alternative Dispute Resolution) kwa kuwa hurahisisha umalizikaji haraka wa mashauri pamoja na kuondoa uadui kwa wadaawa kwani humfanya kila mdaawa kuwa mshindi wa kesi (win-win situation).

 Akizungumza na wananchi kupitia maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Mwinyi amepongeza pia ushirikiano uliopo kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama Zanzibar. Amesema kitendo ya Jaji Mkuu wa Tanzania na ujumbe wake kufika Zanzibar na kuhudhuria maadhimisho hayo ni dalili tosha za kuimarika kwa ushirikiano.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amesema kuwa katika mwaka uliopita 2023, Mahkama ya Zanzibar iliendesha jumla ya mashauri 11,817 yaliendeshwa na Mahakama ambapo kati ya mashauri hayo, mashauri ya jinai yalikuwa 6,944 na mashauri ya madai yalikuwa 4,873.

“Mhe. Mgeni Rasmi katika kipindi hicho, mashauri 8,353 yalisikilizwa na kutolewa uamuzi saw ana asilimia 70.7 ambapo mashauri yanayoendelea Mahkamani ni 3,464, aidha mchanganuo wote wa hali ya usikilizaji wa mashauri kwa Mahkama mbalimbali za Zanzibar umeelezwa kwa kina katika ripoti ya utendaji kazi,” amesema Jaji Mkuu huyo.

Hata hivyo, Mhe. Abdalla amesema kuwa, ufanisi katika shughuli za Mahkama na utoaji wa haki unategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa fedha za kutosha, ambapo ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Mahkama ilipangiwa kutumia jumla ya shilingi 12,911,500,000/- kwa kazi za kawaida na katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Februari 2024 imepanga kutumia jumla ya shilingi 8,835,663,000/- na hadi kufikia mwezi huu Mahkama imeingiziwa jumla shilingi 6,858,781,963 sawa na asilimia 77.6  

Katika kuendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya Mahkama yenye lengo la kuboresha huduma za utoaji haki, Mahkama ya Zanzibar imekamilisha kutayarisha Mpango Mkakati wa miaka mitano (2024/2025-2028/2029) ambao utakuwa muelekeo wa Mahkama hiyo kwa miaka mitano ijayo.

Mhe. Abdalla ameeleza kuwa, kwa mwaka huu Mahkama ya Zanzibar imedhamiria kutia mkazo katika kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha ujenzi wa majengo saba (7) ya Mahkama ulioanza mwaka uliopita, kuendeleza ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi katika utekelezaji wa majukumu.

Vingine ni kuendelea kusimamia kwa ukamilifu nidhamu na maadili kwa watumishi wa Mahkama na Mawakili wa Kujitegemea, kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri na kutolewa uamuzi, kuendelea na maboresho kwa kufanya kazi kwa uwazi na kutoa huduma bora kwa wananchi na mengine.

Maadhimisho hayo yalipambwa kwa shamrashamra kadhaa ikiwemo igizo, mashahiri, kadhalika Rais Mwinyi pia amezindua Mpango Mkakati wa Mahkama ya Zanzibar. Vilevile, katika hafla hiyo Viongozi mbalimbali walipewa nafasi ya kuwasilisha salamu, wakiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar, Mkurugenzi wa Mashtaka Visiwani humo.

Viongozi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria maadhimisho hayo ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.  Mustapher Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda, Kaimu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza, Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na Wasaidizi wa Viongozi hao.

 

Comments (0)

Leave a Comment