Post Details

RAIS SAMIA AONGOZA WATANZANIA KUADHIMISHA SIKU YA SHERIA

Published By:Mary C. Gwera

Akoshwa tena na Kwaya ya Ng’aring’ari

  • Aahidi kuishindanisha na Kwaya ya Bunge, Utumishi wa Umma

Na FAUSTINE KAPAMA -Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan jana tarehe 1 Februari, 2024 amewaongoza Watanzania kuadhimisha Siku ya Sheria na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa mageuzi makubwa ambayo yamefanyika katika kutoa huduma za haki kwa wananchi.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini hapa yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Majaji wa Mahakama ya Rufani.

Alikuwepo pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Eliezer Mbuki Feleshi, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Silvester Kainda pamoja na watumishi wengine.

Wageni wengine walikuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Mawaziri wengine.

Walikuwepo pia Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wastaafu wa Mahakama na Serikali, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Bw. Harold Sungusia na wananchi kwa ujumla.

Rais Samia aliwasili katika Viwanja vya Chinangali majira ya saa 3:10 hivi asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.  Ibrahim Hamis Juma pamoja na Viongozi wa Mahakama na Serikali. 

Baada ya kufika jukwaa kuu Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki ulipigwa kabla ya Mshereheshaji Mkuu, ambaye ni Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza kuwakaribisha Viongozi wa Dini kuyaweka maadhimisho hayo mbele za Mungu.

Kabla ya Jaji Mkuu wa Tanzania kupanda jukwaani kuongea na Watanzania, Mhe. Kahyoza alikaribisha kikundi cha Kwaya ya Mahakama, maarufu Ng’aring’ari ambacho kilikonga nyoyo za Rais na wananchi waliokuwa wamefurika katika Viwanja vya Chinangali. 

Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wabunge na wananchi wengine walishindwa kujizuia, wakaamua kuachia viti vyao na kujimwaga uwanjani kufuatia burudani safi ya nyimbo iliyokuwa inatolewa na kwaya hiyo.

Nyimbo za Kwaya ya Mahakama, hususan zinazoelezea kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Sheria mwaka 2024, masuala ya wosia na dhamana ambao wananchi waliaswa kuacha kuchangishana fedha ili kupata dhamana polisi au mahakamani ziliwaacha wananchi wakitabasamu muda wote kutokana na ujumbe bora wa nyimbo hizo. 

Wakati anazungumza na Taifa kwenye maadhimisho hayo yaliyokuwa yanarushwa mubashara na vituo mbalimbali vya runinga, Rais Samia alitangaza kuanzisha mashindano ‘ligi’ ya Kwaya za Mihimili yote mitatu ya Serikali, yaani Mahakama, Bunge na Serikali.

“Nilikuwa namnong’oneza Spika wa Bunge hapa, nitaanzisha ligi ya kwaya zetu kutoka Mihimili mitatu ya Serikali. Mimi nitadhamini ligi hii ili tuone nani zaidi kati ya Kwaya ya Mahakama, Bunge na Utumishi wa Umma, kazi kwenu,” Rais Samia alisema, huku kauli yake ikipokelewa kwa makofi na vigeregere kutoka kwa wananchi.

Katika kukamilisha maadhimisho hayo ya Siku ya Sheria yanayoashiria mwaka mpya wa shughuli za kimahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania alikagua gwaride maalumu lililokuwa limeandaliwa na Jeshi la Polisi kwa heshima yake na kwa ajili ya shughuli hiyo.

Comments (0)

Leave a Comment