Post Details

PROF KABUDI ATEMBELEA MAONESHO YA WIKI YA SHERIA DODOMA

Published By:Mary C. Gwera

  • Aisifu Mahakama kwa maboresho
  •  Aiomba Mahakama kuandika andiko/kitabu cha historia ya Mahakama Kuu ilipotoka, ilipo na inapoelekea

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi ameisifu Mahakama ya Tanzania kwa hatua ya maboresho iliyopiga inapoadhimisha miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kukagua mabanda ya Mahakama na Wadau wa Mahakama walioshiriki katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania mapema Jan 29, 2021, Prof. Kabudi amesema kuwa kumekuwa na mabadiliko ya dhahiri ndani ya Mahakama ikiwemo miundombinu bora ya majengo yake, teknolojia na kadhalika.

“Nimekagua mabanda nimeona na kufurahishwa na jinsi Mahakama ilivyopiga hatua, ombi langu ni kuangalia jinsi ya kuandika kitabu kitakachoonyesha historia ya Mahakama Kuu katika kipindi cha miaka 100 ilipotoka, ilipo na inapoelekea,” alisema.

Kwa upande mwingine, Waziri Kabudi ameishauri Mahakama inapoendelea na safari ya matumizi ya TEHAMA isisahau pia kuweka kumbukumbu muhimu.

“Si kwamba nakataa matumizi ya teknolojia, bali natoa angalizo pia ya kuweka kumbukumbu na taarifa muhimu kama ‘backup’ kwa ajili ya rejea kwa vizazi vijavyo na kuweka historia nzuri kwa ajili ya Taasisi,” alisema Prof. Kabudi.

Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania yamehitishwa leo Januari 29, 2021 nchi nzima, huku kilele cha wiki hii kikitarajiwa kuwa Februari mosi mwaka huu, ambapo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Katika siku ya mwisho ya maonesho hayo, wageni mbalimbali wamepata fursa ya kutembelea maonesho hayo katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma ikiwa ni pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Magoiga, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na wananchi wengine.

Comments (0)

Leave a Comment