Post Details

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA YATEMBELEA UJENZI WA MAHAKAMA MBEYA

Published By:Mary C. Gwera

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wameanza ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Tanzania inayoendelea nchini ambapo leo wajumbe hao wametembelea miradi iliyopo wilayani Rungwe pamoja na Uyole jijini Mbeya.

Pamoja na wajumbe wa kamati hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. Robert Makaramba pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Sifuni Mchome pia walikuwa ni miongoni mwa viongozi walioshiriki kwenye ziara hiyo.

Katika ziara hiyo mkoani Mbeya, wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walianza ziara yao kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya wilaya ya Rungwe ambao bado uko katika hatua za awali.

Mradi huu uliopangwa kutekelezwa mwaka 2017/2018 unahusisha huduma za mahakama ya wilaya na ya Mwanzo mjini Rungwe ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/S Moladi Tanzania Ltd na kusimamiwa na Chuo kikuu cha Ardhi kama Mtaalamu Mshauri.

Aidha, Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya wilaya na Mahakama ya Mwanzo Rungwe mjini ulianza kutekelezwa mwaka jana na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili mwaka huu.

Baada ya kutembelea ujenzi wa Majengo ya Mahakama wilayani Rungwe, wajumbe wa Kamati hiyo pia walitembelea ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Uyole ulioanza kutekelezwa Desemba 2018 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi April mwaka huu.

Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi M/S PIM Innovators na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoa wa Mbeya kama Mtaalamu Mshauri. Hatua iliyofikiwa sasa ni kuezeka na kuanza kazi za umaliziaji (finishing).

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pia wanatarajia kutembelea na kukagua ujenzi wa Mahakama katika mkoa wa Arusha na Manyara.

Comments (0)

Leave a Comment