Post Details

WIKI YA SHERIA NA MIAKA 100 YA MAHAKAMA KUU KUADHIMISHWA DODOMA

Published By:LYDIA CHURI

  • Jaji Mkuu atoa wito kwa wananchi kuitembelea Tovuti ya Mahakama

Na Lydia Churi- Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma ametoa wito kwa wananchi kujenga mazoea ya kuitembelea Tovuti ya Mahakama ya Tanzania mara kwa mara ili wawe na uelewa mpana wa masuala ya kisheria hasa wanapotaka kufungua mashauri mahakamani au kukata rufaa.

Akizungumza na Waandishi wa leo kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Mkuu amesema tovuti ya Mahakama imesheheni taarifa muhimu ambazo wananchi wakizipata zitasaidia haki kupatikana kwa urahisi.

“Nawaomba Watanzania wakumbuke kuwa wanaweza kupata taarifa wakati wowote ule kuhusu shughuli za Mahakama kwa kutembelea Tovuti ya Mahakama, wananchi wakiwa na tabia ya kuelewa masuala hayo itasaidia upatikanaji wa haki kwa wakati”, alisisitiza Jaji Mkuu.

Kwa mujibu wa Prof. Juma, moja ya malengo matano ya Dira ya Taifa ya  maendeleo 2025, ni kuwepo kwa jamii iliyoelimika na inayojifunza. Aliongeza kuwa taifa linalojifunza ni lile ambalo wananchi wake, kwa juhudi zao, wanatafuta taarifa na elimu wao wenyewe bila kusubiri vyombo vya habari.

Kuhusu maadhimisho ya wiki ya Sheria, Jaji Mkuu alisema wiki hiyo itatanguliwa na matembezi yatakayofanyika tarehe 24/1/2021 yatakayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Alisema matembezi hayo yataanzia Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma na kuishia kwenye viwanja vya Nyerere ambapo yatawakutanisha pia wadau mbalimbali wa Mahakama.

Alitoa wito kwa wananchi wa Dodoma, maeneo ya jirani pamoja wananchi wote wa Tanzania wenye malalamiko, maoni na mapendekezo ya uboreshaji wa huduma za Mahakama wafike kwenye maonesho ya wiki ya sheria ili kupata ufumbuzi.

Alifafanua kuwa wananchi watakaotembelea mabanda ya Mahakama watapata fursa ya kujifunza kwa kiasi gani Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika Karne ya 21 kwa ufanisi kwa matumizi ya TEHAMA.

Baadhi ya mambo yatakayotolewa elimu ya Sheria ni pamoja na taratibu za ufuanguaji wa mashauri, Sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, ndoa na talaka, utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto na taratibu za mashauri ya mirathi.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, elimu itakayotolewa pia itahusu msaada wa kisheria, ushughulikiwaji wa malalamiko mbalimbali na kupokea maoni na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha shughuli za Mahakama na sekta nzima ya sheria, mifumo ya TEHAMA katika uendeshaji wa mashauri na maboresho ya Sheria na Kanuni.

Jaji Mkuu alisema kilele cha maadhimisho ya siku ya Sheria nchini kitafanyika Februari 1, 2021 katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma. Kauli mbiu ya wiki ya sheria ni “Miaka 100 ya Mahakama Kuu: Mchango wa Mahakama katika Kujenga Nchi inayozingatia Uhuru, Haki, Udugu, Amani na Ustawi wa wananchi 1920-2020

Sambamba na elimu ya sheria itakayotolewa kwenye Maonesho yatakayofanyika kitaifa mkoani Dodoma kuanzia Januari 23 hadi 29, 2021, elimu ya sheria pia itatolewa katika Kanda za Mahakama Kuu, Mikoa na Wilaya nchi nzima kama ilivyofanyika kwa miaka mingine.

Katika maonesho hayo, elimu hiyo itatolewa na waheshimiwa Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, na Mahakimu pamoja na wadau wa Mahakama wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na wengine.

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment